27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 12, 2024

Contact us: [email protected]

Sababu ya TRA kuwatoza kodi washereshaji  

2NA KOKU DAVID, DAR ES SALAAM

MIONGONI mwa kazi ambazo huwaingizia watu faida kubwa ni ushereheshaji.

Watu wengi wamejikuta wakijenga majumba, kusoma watoto shule za gharama kwa kazi ya kuongoza sherehe na kufurahisha watu majukwaani.

Watu hawa awali walikuwa hawalipi kodi lakini sasa wametakiwa kulipa kwa sababu imeonekana kuwa ni biashara kama zilivyo nyingine na zinafaida kubwa kwa wahusika.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetakiwa kuongeza mapato ya kodi hadi kufikia Sh trilioni 12.3 kwa mwaka wa fedha wa 2015/16.

Ili kufikisha kiasi hicho cha fedha na kuvuka lengo, ni muhimu kutafuta njia mbadala.

Kwa sababu hiyo, imeamua kuwaingiza wafanyabiashara mbalimbali kwenye sheria ya kodi.

Miongoni mwa wafanyabiashara hao ni pamoja na washereheshaji katika sherehe (MC), wapambaji, wapishi na watoa burudani katika sherehe hizo (DJ).

Katika kuhakikisha inafikia lengo, walikutana na washereheshaji katika sherehe mbalimbali ili kuweza kuwaelimisha kuhusu sheria mpya ya kodi ya ongezeko la thamani iliyoanza kutumika tangu Julai, mosi mwaka jana.

Ofisa Mwandamizi wa Elimu na Kodi wa TRA, Hamisi Lupenja, anasema kila mfanyabiashara anatakiwa kuzijua vizuri sheria zote za kodi ikiwamo ya ongezeko la thamani.

Anasema katika kuhakikisha kila mfanyabiashara anazijua sheria za kodi, TRA imekuwa na utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara kwa ajili ya kuwapatia mafunzo mbalimbali ikiwamo umuhimu wa mashine za EFDs.

“Kila mfanyabiashara anatakiwa kutumia mashine za kodi za kielektroniki yaani EFDs ambazo zitamsaidia kutunza kumbukumbu za biashara zake,” anasema Lupenja.

Anasema si washereheshaji pekee wanatakiwa kulipa kodi bali  sheria ya kodi inamtaka mtu yeyote atakayeuza nyumba, shamba au biashara yoyote inayoingiza kipato kulipa kodi.

“Kabla ya mtu kuuza nyumba au kiwanja chake lazima atamshirikisha mwenyekiti wa mtaa ambaye ndiye atakayetoa taarifa za biashara hiyo kwa TRA na sisi tutaenda kuchukua kodi kama sheria inavyosema,” anasema Lupenja.

Naye Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, anasema TRA imejipanga kuhakikisha inakusanya kodi kutoka sehemu zote zinazostahili kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria.

Anasema walikutana na washereheshaji ili kuwapa mafunzo kuhusiana na namna  wanavyoweza kushiriki kulipa kodi.

“Tunataka elimu hii ya kodi ienee nchi nzima na tunawatoa hofu ya kutotozwa kodi kubwa au kuombwa rushwa, jambo hili litakuwa likifanyika kwa uwazi,” anasema Kayombo.

Anasema TRA inafanya utaratibu wa kuyaingiza makundi mbalimbali katika wigo wa kodi ili kuhakikisha wanalipa kodi stahiki ambazo ndizo zitakazoisaidia nchi kupiga hatua katika masuala ya maendeleo.

Rukia Mtingwa ambaye ni mshereheshaji, anasema washereheshaji walikuwa hawajui ni kwa jinsi gani wanaweza kuchangia katika pato la Taifa kwa kulipa kodi, hivyo wakalazimika kuiomba TRA kuwapa elimu ya kodi ili waweze kuchangia kulingana na kazi wanazofanya.

Anasema hakuna mshereheshaji asiyetaka kulipa kodi bali walikuwa hawajui sheria za kodi zinasemaje na zinataka nini.

Pia anasema TRA ilikuwa haijui washereheshaji wawaweke katika kundi gani hasa ikizingatiwa kuwa hata kipato wanachokipata kwa mwaka hakifahamiki.

“Baada ya mafunzo haya sisi tupo tayari kulipa kodi, pia tunaomba wateja wetu watuelewe pindi tutakapokuwa tunatoa bei na wakumbuke kutuomba risiti ili kodi yao iweze kufika TRA,” anasema Rukia.

Naye Lameck Matemba ambaye pia ni mshereheshaji, anasema kulipa kodi ni jambo zuri kwa maendeleo ya nchi hivyo watu wote watakaokuwa na sherehe wanatakiwa kufanya kazi na washereheshaji wanaolipa kodi.

“Tunapita kwenye barabara nzuri kwa sababu ya kodi, tunataka watoto wetu wasome vizuri hivyo tunatakiwa kujifunza kuipenda nchi yetu kwa kuitumikia ikiwa ni pamoja na kulipa kodi,” anasema Matemba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles