WAKATI uchaguzi wa klabu ya Yanga unatarajia kufanyika mwezi ujao, zoezi la uchukuaji fomu limeonekana kudorora kwani mpaka sasa wamejitokeza wagombea wawili tu kuchukua fomu hizo tangu zoezi hilo lianze Mei 25 mwaka huu.
Zoezi hilo la kuchukua fomu lilitarajiwa kumalizika leo lakini kwa taarifa zilizopatikana linaweza kusogezwa mbele kwa siku mbili ili watu wajitokeze.
Wagombea waliojitokeza katika zoezi hilo hadi sasa ni wale wa nafasi ya Ujumbe wa Kamati Tendaji ya klabu hiyo, ambao ni Pascal Raizer na Edgar Chibula.
Uchaguzi huo unatokana na agizo la Baraza la Michezo la Tanzania ‘BMT’, kulitaka Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ kusimamia zoezi hilo kwa mujibu wa katiba na sheria.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF chini ya Mwenyekiti wake, Aloyce Komba, zilisema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya zoezi hilo kuonekana kusuasua.
“Zoezi hili litaongezwa siku mbili kuanzia sasa, kwani ni vigumu kumalizika leo kutokana na wagombea kushindwa kujitokeza kwa wingi.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa hali hiyo inatokana na klabu hiyo kugawanyika makundi mawili makubwa ambayo yanategeana katika kufanikisha zoezi hilo.
“Tunatarajia wagombea wengi wa nafasi mbalimbali kuanza kujitokeza leo, kutokana na kutegeana kuchukua fomu hizo,” kilisema chanzo hicho.