26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, November 21, 2024

Contact us: [email protected]

Mambo ya kuzingatia ili kupata wawekezaji

Na Makirita Amani

MTAJI wa fedha ni muhimu katika kuanza au kukuza biashara. Inawezekana ukawa na mtaji kidogo au mkubwa kulingana na wazo la biashara ulilonalo. Wajasiriamali na wafanyabiashara wengi hawana kiasi cha fedha cha kutosha kuanzisha au kukuza biashara zao. Hii inasababisha kuhitajika kwa njia mbadala za kuweza kupata mtaji.

Kuna njia nyingi ambazo mtu anaweza kuzitumia kupata mtajikama kupitia mikopo kutoka taasisi za kifedha, mchango kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki au kutoka kwa wawekezaji. Leo tutajadili fedha kutoka kwa wawekezaji kama njia ya kupata mtaji.

Kwanza kabisa ni vyema tukamjua mwekezaji ni mtu wa aina gani. Mwekezaji ni mtu ambaye ana fedha ambazo anaweza kuziweka kwenye biashara mbalimbali na zikazalisha. Huwa hatoi fedha kama mkopo, bali naye huwa anakuwa sehemu ya umiliki wa biashara. Anapowekeza kwenye biashara yako maana yake unampa hisa, hivyo unapopata faida na yeye anapata faida kulingana na mtaji alioweka. Kama utapata hasara basi na yeye atapata hasara.

Kutokana na changamoto hii ya kupata hasara, wawekezaji wapo makini na uwekezaji wa fedha zao. Hawaweki fedha zao kwenye kila biashara, wana vigezo ambavyo wanaviangalia. Hapa tutaviangalia vigezo hivi ili uweze kuvizingatia kama unataka kuvutia wawekezaji.

Wawekezaji wanavutiwa kuwekeza kwenye biashara ambayo inaendeshwa kitaalamu na kisheria. Kuna biashara nyingi ambazo zinafanya vizuri lakini zinakosa watu wa kuwekeza kwa sababu zinaendeshwa kwa mazoea. Biashara haijasajiliwa na hakuna utaratibu wowote wa uendeshaji.

Hakuna mtu anayeweza kuweka fedha zake kwenye biashara ya aina hii kwa sababu anajua zitapotea. Makubaliano mnayoingia na mwekezaji ni ya kisheria na hivyo lazima biashara iwe inatambulika kisheria. Unahitaji kuisajili kama kampuni au jina la biashara. Pia uwe unalipa kodi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Wawekezaji wanahitaji mchanganuo wa biashara, unaoonesha biashara inahusu nini, wateja ni kina nani, wanapatikanaje na mipango ya ukuaji wa biashara hiyo. Mambo haya yanatakiwa yawe yameandikwa na kuwekewa mikakati ili kuyafikia. Unaweza kuwa na mipango mizuri kuhusu biashara yako lakini kama hujaiandika vizuri kwa njia ambayo mtu anaweza kuelewa, itakuwa vigumu kupata wawekezaji. Mara nyingi mwekezaji hakujui wewe moja kwa moja, hivyo njia kuu ya kumshawishi ni kuwa na nyaraka hizi muhimu.

Usimamizi mzuri ni kitu ambacho wawekezaji wanakithamini. Kwa kuwapo kwa usimamizi mzuri wanakuwa na uhakika kwamba fedha wanazowekeza zitasimamiwa vizuri na kuleta faida ambayo itawafaidisha na wao pia. Unahitaji kuwa na usimamizi mzuri wa biashara yako, usimamizi ambao una historia nzuri ya kufanya maamuzi yenye manufaa kwenye biashara yako.

Ni muhimu biashara ikawa na vitengo ambavyo vinasimamia yale maeneo muhimu ya biashara kama masoko, uzalishaji, mauzo na kadhalika. Hata kama bado hujaweza kuajiri watu wa kukusaidia, kuwa na mpango mzuri kutawashawishi wawekezaji waone unaweza kufanya vizuri.

Wawekezaji wanapendelea kuwekeza kwenye biashara ambayo tayari imeshaanza. Watu wengi wamekuwa wakiandaa mawazo mazuri na kuwaomba watu wawekeze kwenye mawazo hayo ya kibiashara. Lakini kuandaa wazo ni kitu rahisi, unaweza kumlipa mshauri wa biashara akakuandalia wazo zuri.

Wawekezaji wengi wanapendelea kuwekeza kwenye biashara ambazo tayari zimeshaanza. Hapa wanaweza kuzifuatilia na kuona zinafanya vizuri na hivyo kuweka mitaji yao. Kama una wazo kubwa la biashara ambalo unahitaji kupata wawekezaji, anza kidogo na waoneshe kwamba wazo hilo linawezekana. Kwa njia hii wengi watashawishika.

Kuna watu wengi ambao wana mitaji yao ila hawajaweza kuiweka kwenye biashara za wengine kwa kuhofia usalama wa mitaji hiyo. Kama ukiweza kuiweka biashara yako vizuri unaweza kuwashawishi watu hawa na wote mkanufaika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles