25.6 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

TBL na Tanzania Red Cross wazindua mpango wa mafunzo kwa waendesha pikipiki kupunguza ajali barabarani

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Tanzania Breweries Limited (TBL), kwa kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS), imezindua mpango wa mafunzo na elimu kwa waendesha pikipiki wenye lengo la kuboresha usalama barabarani na kupunguza ajali zinazohusisha pikipiki.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin, alieleza kuwa mpango huo ni sehemu ya juhudi za kampuni katika kuunga mkono Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG), hasa lengo la kupunguza idadi ya vifo na majeraha yatokanayo na ajali za barabarani ifikapo mwaka 2030.

“Tanzania Breweries Limited inaunga mkono lengo la maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa la kupunguza vifo na majeraha kutokana na ajali za barabarani. Tunaamini kampuni yetu ina nafasi ya pekee kuboresha usalama barabarani na kuleta mabadiliko chanya katika jamii zetu,” alisema Kilpin.

Aliongeza kuwa, mpango huo, ambao utaendeshwa kuanzia Septemba hadi Desemba 2024, unalenga kupunguza ajali za barabarani kupitia programu ya kina ya elimu na mafunzo kwa waendesha pikipiki. “Mpango huu ni sehemu ya Kampeni ya Smart Drinking na ni kipaumbele kwetu kutokana na ukweli kwamba wenzetu, familia zao, na wateja wetu wanasafiri barabarani kila siku.” amesema Kilpin.

Kilpin alifafanua kuwa waendesha pikipiki wanaotoa huduma za usafiri katika wilaya za Kinondoni, Ubungo, Ilala, na Temeke jijini Dar es Salaam ndio walengwa wakuu wa mpango huo. “Tutawafikia waendesha pikipiki hawa kupitia vyama vyao vilivyopo katika wilaya hizi nne.”.

Ameongeza kuwa mpango huo utabuni na kutekeleza mtaala maalum wa mafunzo, kuanzisha ushirikiano na shule za uendeshaji, pamoja na kuendesha kampeni za uhamasishaji wa jamii. “Zaidi ya hayo, tunalenga kuongeza uelewa wa huduma za kwanza miongoni mwa waendesha pikipiki ili kuimarisha uwezo wao wa kusaidia wahanga wa ajali.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Shirika katika TRCS, Reginald Mhango, alieleza umuhimu wa mpango huo, akisema ongezeko la ajali za pikipiki nchini Tanzania ni tatizo linalohitaji utatuzi wa haraka. “Mradi huu umelenga kushughulikia changamoto hizi kupitia elimu na mafunzo ya kina, na hatimaye kupunguza vifo na majeraha.”

Mhango aliongeza kuwa mradi unalenga kupunguza ajali za barabarani zinazohusisha pikipiki kwa asilimia 30 ndani ya miaka mitatu, na kushirikisha waendesha pikipiki wapatao 10,000 nchini Tanzania katika kipindi cha miaka miwili ya kwanza. “Tunalenga kuimarisha uelewa wa waendesha pikipiki kuhusu sheria za usalama barabarani kwa asilimia 50 ndani ya mwaka wa kwanza.”

Ili kufanikisha malengo hayo, mradi huu utashirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo mamlaka za serikali za mitaa, vyama vya waendesha pikipiki, vikosi vya polisi, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), na viongozi wa jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles