23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi wa Chidachi Kusini waomba Kupimiwa maeneo yao, watupia lawama ofisi ya Jiji na mbunge

Na Ramadhani Hassan, Mtanzania Digital

Wananchi wa Mtaa wa Chidachi Kusini, jijini Dodoma, wametoa wito kwa Mbunge wa Jiji la Dodoma na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, kushirikiana na ofisi ya Jiji la Dodoma ili kuwapimia maeneo yao kwa ajili ya kuendeleza ujenzi, wakilalamikia changamoto hiyo kuwa tatizo la muda mrefu.

Wakizungumza na waandishi wa habari Septemba 24, 2024, wananchi hao wamesema kuwa waliahidiwa kupimiwa maeneo yao tangu mwaka 2018, lakini hadi sasa hakuna hatua zilizochukuliwa wala mawasiliano yoyote yaliyotolewa. Magreth Dossa (66), mkazi wa Chidachi Kusini tangu utoto wake, alisema wamekuwa wakizungushwa kwa miaka mingi bila mafanikio.

“Mwaka 2018 walikuja kutuhakiki, tukadhani mambo mazuri yanakuja. Lakini tangu kipindi hicho hadi sasa, hatujapimiwa na hakuna anayesema chochote,” alisema Dossa. Aliongeza, “Wenzetu wa Chidachi Senta wamepimiwa, tunashangaa sisi kwanini hawajatufikia. Ina maana sisi siyo Watanzania? Tunastahili kupimiwa, lakini hakuna anayejibu barua tulizoandika.”

Maria Mwanza, mkazi mwingine wa eneo hilo, alieleza kuwa eneo la Chidachi Kusini ni la asili na wanaiomba Serikali pamoja na timu ya mipango miji kuja na kupima maeneo yao. “Tunashindwa kuendeleza maeneo yetu. Hali hii inalazimisha sisi na watoto wetu wakubwa kulala kwenye chumba kimoja. Tunawafundisha nini hawa vijana wetu?” alihoji Mwanza.

Issa Lazaro, mkazi wa eneo hilo, aliongeza kuwa hali ni mbaya kwa familia nyingi, ambazo zinakosa nafasi ya kujenga nyumba zao kwa sababu ya kutokupimiwa maeneo. Aliomba msaada kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma. “Tunahitaji upanuzi wa makazi. Tukipimiwa, tutapata hati, na hii itatusaidia hata kukopesheka kwenye taasisi za kifedha,” alisema Lazaro.

Shabani Kayanda aliongeza kuwa licha ya jitihada zao, hakuna mafanikio yaliyopatikana hadi sasa. Alifafanua kuwa, “Eneo hili lina huduma zote muhimu kama misikiti, makanisa, na umeme wa Rea, lakini zoezi la upimaji limekuwa changamoto.” Alibainisha kuwa eneo lililokuwa na kaya zaidi ya 600 limegawanywa, na sasa kaya 130 pekee ndizo zinazoomba kupimiwa.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Chidachi Kusini, Mohamed Msanga, alithibitisha madai ya wananchi, akieleza kuwa upimaji ulianza tangu mwaka 2014, lakini baadhi ya maeneo yalipimwa huku mengine yakiwekwa kando. “Watu wengi wamejenga nyumba nzuri lakini hawana hati, na hali hii inailazimisha Serikali kupoteza mapato kwa miaka mingi,” alisema Msanga. Aliongeza kuwa, tatizo hilo lilianzishwa na Mamlaka ya Ustawishaji na Mipango Miji (CDA), ambayo iliacha mgogoro huo bila suluhisho, na sasa ofisi ya jiji imekuwa haitoi ushirikiano wa kutosha.

Juhudi za kumtafuta Maduhu Ilanga, Mkuu wa Divisheni wa Uendelezaji wa Makao Makuu kwa ajili ya kutoa ufafanuzi, hazikuzaa matunda kwani simu yake iliita bila kupokelewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles