Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Rais Samia Suluhu Hassan amesikiliza kilio cha wakazi wa Tarafa ya Ngorongoro na ameagiza kurejeshwa kwa huduma za kijamii, ikiwemo elimu na afya, ambazo zilikuwa zimesitishwa katika eneo hilo.
Agizo hilo limetolewa leo, Ijumaa, Agosti 23, 2024, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata 11 zilizopo katika Tarafa ya Ngorongoro. Waziri Lukuvi alifika eneo hilo kwa niaba ya Rais Samia, baada ya wakazi hao kukusanyika na kukesha kwa siku tano wakitaka majibu kuhusu malalamiko yao.
Pamoja na kurejesha huduma hizo, Rais Samia pia ameagiza kwamba uchaguzi katika tarafa hiyo ufanyike kwa kutumia mipaka ya zamani, kama inavyofanyika katika maeneo mengine nchini.