24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, September 19, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia ataka falsafa ya 4R itumike sekta ya ushirika

*Aagiza maofisa ugani wapimwe kwa utendaji

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza maofisa ugani wapimwe kwa utendaji wao huku pia akitaka falsafa ya kujenga upya, maridhiano, ustahimilivu na mabadiliko (4R) itumike kukuza sekta ya ushirika nchini.

Amesema mwelekeo wa serikali ni kujenga uchumi jumuishi unaochechea maendeleo vijijini na kuongeza kasi ya kupunguza umaskini kwa wananchi hivyo maofisa ugani na maofisa ushirika wana umuhimu mkubwa katika kutimiza azma hiyo.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan akizungumza na maofisa ugani na wanaushirika Ikulu Chamwino, jijini Dodoma.

Akizungumza leo Agosti 10,2024 wakati wa kikao kazi na maofisa ugani na maofisa ushirika kilichofanyika Ikulu Chamwino jijini Dodoma amesema anataka kuacha alama kuhakikisha vyama vya ushirika vinasimama vyenyewe kwa maendeleo ya wakulima.

“Ushirika unatakiwa uwe mtetezi na msimamizi wa wana ushirika, sio uwe mbinyaji na mkandamizaji wa haki ya mwana ushirika, tuliyokuwa tukiyasikia hayaleti picha nzuri. Tunataka vyama vya ushirika vikisimama visemwe duniani kote, R4 zifanye kazi kwa wana ushirika wote ili sekta hiyo isimame vizuri,” amesema Rais Samia.

Rais Samia pia ameahidi kutoa Sh bilioni 5 kununua hisa za serikali ili kuharakisha uanzishwaji wa Benki ya Ushirika nchini.

Kuhusu maofisa ugani amesema serikali imeboresha mazingira yao ya kazi kwa kuwaongezea uwezo wa kuwafikia wananchi ambapo imewapelekea pikipiki, magari na vishikwambi.

“Maofisa ugani ni mashujaa wasiosemwa na mtu lakini uhakika wa chakula tunaojivunia kwa asilimia 128 unatokana na maofisa ugani, niliwashukuru wakulima kwa sauti kubwa lakini leo ni siku ya kuwashukuru ninyi kwa sauti kubwa pia,” amesema Rais Samia.

Amemtaka Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kuhakikisha wakala wa ugani unaanzishwa na jukumu mojawapo liwe ni kuwapima wataalam hao.

Mwenyekiti wa Maofisa Ugani Tanzania, Enock Ndunguru, amesema kuunganishwa Idara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika serikali za mitaa kunachangia changamoto katika sekta ya ugani na kuomba zitenganishwe.

Amesema changamoto nyingine ni uchache wa maofisa ugani na kushauri kila kijiji kiwe na ofisa ugani wa kilimo au mifugo ili kuongeza tija tofauti na ilivyo sasa ambapo waliopo hawazidi 6,800 wakati mahitaji ni zaidi ya 20,000.

Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema wamekuwa wakifanya kazi kwa kuzingatia falsafa nne za kujenga upya, maridhiano, mabadiliko na ustahimilivu.

Amesema walikuwa na malengo saba ambayo yalijikita katika kuimarisha maendeleo ya ushirika na kudhibiti na kusimamia uendeshaji wa shughuli za ushirika na kwamba hadi sasa kuna mabadiliko makubwa.

Amesema pia walifanyia kazi wazo la kuanzisha benki ya ushirika nchini ambapo wana ushirika wametengewa asilimia 51 ya hisa huku malengo yakiwa ni kupata mtaji wa Sh bilioni 20.

Kwa mujibu wa Nsekela, hadi sasa wameshapata Sh bilioni 16.6 na tayari wamepata leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Mohamed Mchengerwa, amesema wameendelea kusimamia na kusisitiza mamlaka za serikali za mitaa kutenga na kutumia asilima 20 ya mapato ya ndani yanayotokana na mazao ya kilimo katika kutekeleza mipango ya maendeleo ya sekta hiyo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amesema maofisa ugani wa mifugo na uvuvi waliopo nchini ni 5,083 na kati yao 4,406 ni wa mifugo na 677 ni wa uvuvi.

Amesema ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia maofisa ugani wa mifugo na uvuvi wamepata pikipiki 2,762 na kwamba wametenga Sh bilioni 28 kwa ajili ya kuchanja mifugo nchi nzima.

Amesema wizara hiyo pia imetoa mafunzo rejea kwa maofisa 3,600 na kati yao 3,100 ni wa mifugo na 500 wa uvuvi kuhusu teknolojia mbalimbali na maarifa ya kisasa.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema wakati Rais Samia anaingia madarakani bajeti ya ugani ilikuwa Sh milioni 682 na kwa sasa imeongezeka na kufikia Sh bilioni 17.07.

Amesema pikipiki zilizonunuliwa kwa maofisa kilimo zimefikia 6,800, magari 46 ambapo pikipiki zimefungwa mfumo maalumu zikiibiwa inakuwa rahisi kuzikamata. Amesema wameshanunua vishikwambi 4,400 ambavyo vitawawezesha maofisa ugani kuandaa takwimu sahihi za mkulima na shamba.

Amesema pia wameshagawa vipima afya ya udongo katika halmashauri 143 na tayari wakulima wameanza kupimiwa na kumpongeza Ofisa Kilimo wa Rungwe kwa kazi nzuri anayofanya.

Kuhusu ushirika amesema viwanda mbalimbali vilivyokuwa vimekufa vimefufuliwa na kuanza kununua mazao ya wakulima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles