25 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

TPDC kuanza uzalishaji wa Gesi Asilia katika Visima vya Ntorya 1 na 2, Mtwara

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na kampuni ya mafuta ya ARA lipo mbioni kuanza uzalishaji wa gesi asilia katika visima vya Ntorya 1 na Ntorya 2 vilivyopo mkoani Mtwara, kata ya Nanguruwe katika kijiji cha Namayhakata Shuleni. Hatua hii ni zao la juhudi za TPDC katika utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

Wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara-Kijiji cha Nanguruwe.

Kwa maandalizi ya uzalishaji, TPDC imejikita katika kutoa elimu kwa jamii pamoja na viongozi wa serikali ngazi zote za mkoa na wilaya. Mikakati hii inajumuisha mikutano ya hadhara na wananchi walioathiriwa na mradi huo. TPDC na ARA wanashirikiana na kampuni mshauri mwelekezi APY-KEGS katika masuala ya tathmini na uthamini wa ardhi ili kuhakikisha utwaaji wa ardhi unafanyika kwa ustadi.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Julai 6,2024 katika kijiji cha Nanguruwe, Meneja Mradi wa Ntorya kutoka TPDC, Patrick Kabwe, amesema:

“Shughuli za uzalishaji kwa visima hivi viwili vya gesi zinatarajiwa kuanza Aprili, 2025, ambapo kila kisima kitakuwa na uwezo wa kuzalisha futi za ujazo milioni 20 kwa siku. Pia tunategemea kuchimba kisima cha tatu kinachoitwa Chikumbi-1 ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha futi za ujazo milioni 20. Kwa awamu ya kwanza, uzalishaji kwa visima vyote vitatu utakuwa jumla ya futi za ujazo milioni 60 kwa siku.

“Aidha, awamu ya pili ya uzalishaji itajumuisha kuchimba visima vinne zaidi katika kata ya Nanguruwe ambapo uzalishaji utafikia futi za ujazo milioni 140 kwa siku,” amesema Kabwe.

Meneja Mradi wa Ntorya Patrick Kabwe.

Katika mkutano huo, Kabwe alishukuru uongozi wa mkoa na wilaya kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika kufanikisha mradi huu.

“Sisi TPDC pamoja na ARA Petroleum tunashukuru serikali ya mkoa na wilaya kwa ushirikiano wanaotupatia kwani bila wao tusingefika hapa. Ushirikiano wanaotupatia ndio unasaidia mpaka sasa mradi unaendelea,” amesema Kabwe.

Mwakilishi wa kampuni ya ARA, Judith Kalugasha, amesema mradi huo wa gesi sio wa kwanza kwa kata ya Nanguruwe na kwamba kinachofanyika sasa ni muendelezo wa miradi iliyopita. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kutoka kwa wananchi ili mradi ukamilike kwa wakati.

Mwakilishi wa Kampuni ya ARA-Judith Kalugasha akitoa ufafanuzi wa jambo katika mkutano wa hadhara –Nanguruwe.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi wa TPDC, Oscar Mwakasege alieleza umuhimu wa miradi ya gesi asilia kwa jamii ikiwemo ajira na uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii kama afya, elimu, maji na utawala bora.

“TPDC tunafanya kazi na jamii hivyo tunawajibika kuleta ustawi wa huduma za kijamii kwenye vijiji tunavyotekeleza miradi ya gesi asilia, ikiwemo kijiji cha Nanguruwe,” alisema Mwakasege.

Diwani wa kata ya Nanguruwe, Patrick Simwinga, alipongeza TPDC na kampuni ya ARA Petroleum kwa kuwa na mpango mzuri wa kushirikisha jamii katika hatua za awali za utekelezaji wa mradi, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kabla ya kuanza mradi.

Muonekano wa Kisima cha gesi asilia Ntorya-2 kilichopo katika kijiji cha Nanguruwe, mkoani Mtwara.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles