27.6 C
Dar es Salaam
Saturday, September 28, 2024

Contact us: [email protected]

Watu 13 wafariki ajarini Mbeya

Na Grace Mwakalinga, Mbeya

Watu 13 wamefariki papo hapo na wengine 18 kujeruhiwa kwenye ajali ya barabarani iliyotokea katika eneo la mteremko wa Mbembela jijini Mbeya baada ya Lori lililokuwa limebeba shehena ya kokoto kufeli breki na kuparamia magari mawili, pikipiki na guta.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Benjamin Kuzaga ambaye alikuwepo eneo la tukio amelitaja lori lililosababisha ajali hiyo kuwa ni aina ya Scania yenye namba za usajili T. 979 CVV na tela lenye namba za usajili T. 758 BEU ambalo lilikuwa linatokea Uyole kuelekea barabara ya Tunduma.

Amesema lori hilo lilianza kuigonga gari ndogo aina ya Harrier yenye namba za usajili T. 120 DEL na kupoteza mwelekeo kwenda kuigonga gari aina ya Coaster yenye namba za usajili T.167 DLF ambayo ilikuwa inatokea Tunduma kuelekea jijini Mbeya.

Ameongeza kuwa mbali na magari hayo, pia lori hilo liliparamia waendesha pikipiki maarufu kwa jina la Bodaboda na guta moja ambalo lilibeba shehena ya mahindi.

Amesema vifo na majeruhi wengi ni waliokuwa kwenye gari la abiria ambalo liliburuzwa mpaka kwenye mtaro na kwamba abiria wengi walikuwa wamebanwa.

“Dereva wa lori tumempata na tunaendelea kufuatilia hawa wa vyombo vingine ili kubaini kama ni miongoni mwa majeruhi ama waliokufa, lakini ile gari ndogo aina ya Harrier limeharibika tu,”amesema Kuzaga.

Baadhi ya wananchi walioshuhudia ajali hiyo wamedai waliona gari hilo likiwa linashuka mlima huo likiwa limewasha taana linapiga honi kuashiria hatari.

Mmoja wa mashuhuda hao, Bashiri Mwaluwanda amesema dereva wa lori hilo alifanikiwa kuyakwepa baadhi ya magari na bajaji kwenye mteremko huo na baada ya kuigonga gari ndogo akapoteza mwelekeo na kuanza kuyumba.

Ameongeza kuwa baada ya kuligonga coasta na kuanguka walianza kuwaokoa baadhi ya waathirika hasa majeruhi na kuwakimbiza hospitali kwa kutumia pikipiki na bajaji kabla ya magari ya kubeba wagonjwa kufika katika eneo hilo.

Amesema baadhi ya watu ambao walikuwa wamebanwa kwenye gari hiyo ya abiria waliondolewa baada ya askari wa kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kufika na vifaa.

“Watu waliofariki ni wengi maana, hata hivyo dereva amejitahidi sana kuyakwepa magari mengine na yaliyokuwa yanapandisha kwenye huu mteremko, yule wa Coaster alishindwa kumkwepa kwa sababu ni eneo la matuta,” amesema Mwaluwanda.

Naye Mapinduzi Mwambambe amesema alipigiwa simu na mdogo wake ambaye anafanya shughuli zake eneo la Simike akamueleza kwamba kuna lori limefeli breki linashuka uelekeo wa Mbembela na akamtahadharisha kwamba kama yuko barabarani aondoke.

Amesema kabla mdogo wake hajamaliza kutoa maelezo hayo alisikia kishindo barabarani na alipokwenda kuangalia akakuta lori hilo limeshagonga gari ya abiria ndipo akaanza kushiriki kwenye uokoaji.

Amesema uokoaji ulikuwa rahisi kwa sababu ni eneo la jeshini na hivyo askari wengi wa kikosi cha Jeshi cha 844 Itende KJ walishiriki kwenye uokoaji pamoja na kutoa taarifa kwenye vyombo vingine vya dola.

Magari manne yalishuhudiwa kubeba wagonjwa, mawili ya Jeshi la Polisi na moja la Jeshi la Wananchi wa Tanzania yakisomba majeruhi na miili ya marehemu kupeleka katika Hospitali ya Kanda ya Rufani ya Mbeya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles