25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yadhamiria kufanya uwekezaji sekta za uzalishaji

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha nchi inakuwa na maendeleo endelevu, kwa kufanya uwekezaji katika sekta za uzalishaji.

Ameyasema hayo leo Februari 29, 2024 jijini Dar es Salaam alipofungua Mkutano wa Majadiliano ya Kimkakati kati ya Serikali na wadau wa maendeleo ngazi ya juu.

Amesema kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuwa na maendeleo endelevu ambayo hayamuachi Mtanzania yoyote nyuma.

“Kipaumbele kimewekwa kwenye uwekezaji katika mtaji wa binadamu, maendeleo ya miundombinu, kuhamasisha ukuaji wa kiuchumi, kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii, utawala bora, kuwawezesha wanawake na uhifadhi wa mazingira,” amesema Dk.Nchemba.

Amesema kwa kutekeleza mikakati hiyo pamoja na kukuza ushirikiano na sekta binafsi, asasi za kiraia na washirika wa maendeleo, Tanzania inaweza kupiga hatua kubwa kuelekea kufikia ukuaji wa uchumi endelevu.

Dk. Nchemba amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuimarisha mazingira ya ukuaji wa biashara, kuongeza ushindani na kukuza ubunifu ili kukuza uchumi wa nchi.

Aidha amesema Tanzania pia inatumia Diplomasia ya Kiuchumi kama mkakati muhimu wa kuendeleza uchumi wake na kubainisha kuwa nchi ina dhamira kubwa ya kufuata kanuni za ushirikiano wa Kimataifa wenye manufaa kwa pande zote.

Kwa upande wake, Balozi wa Uingereza nchini na Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano huo, David Concar, amesema kuwa wadau wa maendeleo wanampongeza Rais, Dk. Samia kwa kazi kubwa anayofanya na wanayaona mabadiliko mbalimbali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji, biashara pamoja na uwekezaji katika sekta ya uzalishaji.

Amesema kuwa wadau wa maendeleo wako tayari kuendelea kuiwezesha nchi kufikia maendeleo ya kukuza uchumi wa wananchi.

” Wadau wa maendeleo wametoa zaidi ya Dola bilioni 2.7 kwa ajili ya kuisaidia Tanzania kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo asilimia 51 ya fedha hizo ni misaada na asilimia 49 ni mikopo yenye masharti nafuu,” amesema Concar.

Amebainisha kuwa asilimia 40 ya fedha hizo zilitolewa na nchi moja moja za washirika wa maendeleo na asilimia 60 za fedha hizo zimetolewa na Taasisi za Kimataifa za fedha ikiwemo Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Nao washiriki wa mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa SRF, Prof. Fortunata Makene na Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Dk. Donald Mmari, wamesema kuwa majadiliano hayo ni muhimu kwa maendelo ya nchi kwa kuwa yanaikutanisha Serikali na wadau wa maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles