Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama ametoa wito viongozi kuhakikisha wanawapatia wenyeviti wa Mashina wa Chama cha Mapinduzi taarifa muhimu za utekelezaji wa Miradi ya maendeleo ili waweze kuzielezea vyema kwa Wananchi.
Waziri Mhagama ametoa kauli hiyo Wakati wa ziara yake ya kutembelea Wenyeviti wa Mashina Katika Kata ya Magagula; Mbingamwalule, Kizuka, Liganga na Litisha zilizopo Jimbo la Peramiho lilopo katika Halmashauri ya Songea Vijijini Februari 27, 2024 Mkoani Ruvuma.
Ameongeza kuwa siasa za sasa zinalenga katika kujenga hoja hivyo ni muhimu wenyeviti wa mashina kuwa na maelezo muhimu yatakayosaidia kukielezea Chama vyema kwa wananchi.
“Utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya CCM inategemea Mafiga Matatu kwa maana ya Rais, Mbunge na Diwani jambo ambalo linarahisisha katika utekelezaji wa shughuli za serikali na heshima hiyo mnatupatia nyie wenyeviti wa mashina,” alisema na kuongeza kuwa:
“Wenyeviti endeleeni kuwa na uelewa mzuri wa miradi inayotekelezwa na Serikali kwani itasaidia kusemea chama na Rais ikiwa ni sambamba na kusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo pamoja,” alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Vijijini, Thomas Masolwa amesema ziara ya mbunge Mhagama kutembelea Wenyeviti wa Mashina inasaidia kujenga na kuimarisha Chama.
Ameongeza kusema kuelekea uchaguzi ujao ni vyema Wenyeviti wa Mashina wakajua kwamba Uchaguzi ni hesabu za namba, ukiwa na namba nyingi lazima utakuwa umemshinda mpinzani wako.
“Ni vyema  tuhamasishe wananchi waende kukipigia kura Chama Cha Mapinduzi, tutengeneze wapiga kura kwa kuhakikisha wanasajiliwa ili watambulike na Chama,” alisema.