23.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Bunge laridhia azimio la Serikali

*Ni kuhusu mkataba wa Tanzania na Dubai

Na Mwandisi Wetu, Mtanzania Digital

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Jumamosi Juni 10, 2023 limekubali na kupitisha Azimio la Bunge juu ya Pendekezo la Kuridhiwa kwa Mkataba baina ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai wenye lengo la kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika uendelezaji wa maeneo ya Bandari nchini.

Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson ametumia nafasi hiyo kuwataka Watanzania kupuuziaupotoshaji unaoendelea katika katika mitandao ya kijamii sababu ina nia ovu na Serikal.

Amesema ni vyema kufanya utafiti wa taarifa wanazopewa kwani makubaliano hayo yanaweza kusitishwa kwa mujibu wa kifungu cha 23 ambacho kinaruhusu upande wowote kusitisha endapo mambo yakienda kinyume.

“Mikataba ipo itakayoingiwa ya uendelezaji na uendeshaji ambayo haiwezi kulingana muda na siyo kupokea taarifa za upotoshaji za mkataba wa miaka 100, na yale mawazo yenu kuhusu muda yatawekwa huko, mtu anaibuka na heshima zake anasema ni wa miaka 100 ameisoma wapi kwenye huu mkataba? hakuna miaka 100 wala mwezi mmoja, kayatoa wapi?,” amehoji Dk. Tulia na kuongeza kuwa:

“Niungane na wabunge ambao wamependekeza Watanzania tujifunze kufanya utafiti ili unapozungumza usiwe sehemu ya wapotoshaji, mkataba umeshasainiwa halafu ndiyo unapelekwa bungeni sasa inakuwaje, halafu wapotoshaji hawajasoma hata ni shughuli gani ambazo wabunge humu ndani mmependekeza,” amesema Dk. Tulia.

Spika huyo wa bunge amefafanua zaidi kuwa kitendo cha azimio hilo kuwasilishwa bungeni hapo ni kwa lengo la kutoa mapendekezo ambayo yataisaidia serikali kufanya utafiti kabla haijakabidhi kampuni DP WORLD itkayoletwa na Serikali ya Dubai na kwamba wao wawe wamefanya utafiti utakaoweka wazi mwelekeo wa wapi imefika na wapi inakwenda na kama kutakuwa na mabadiliko kifungu cha 23 kinaeleza kusitisha.

“Kwamba serikali yetu kabla haijakabidhi Kampuni itakayoletwa na Dubai wao wawe wamefanya utafiti wa kawaida kabisa ili wanapoenda waseme tulikuwa tumefika hapa ninyi mchango wenu ni huu na tunatarajia huu msipoufanya tutakatisha,” amesema Dk. Tulia.

Mapema, akitoa hoja bungeni, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Makame Mbarawa, alisema kuwa hii siyo mara ya kwanza kuwa na mwekezaji katika sekta ya bandari nchini.

“Kuanzia miaka ya 2000, Serikali ya Awamu ya Tatu kupitia Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) iliingia mkataba wa upangaji na uendeshaji (lease and concession agreement) na Kampuni ya Kimataifa ya Uendeshaji wa Vitengo vya Makasha, Hutchison ya Hong-Kong China 9TICTS). Mkataba huo ulidumu kwa miaka 22 kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2022 na uliipa haki ya kipekee kampuni hiyo kwa ajili ya kuendesha shughuli za kuhudumia makasha katika gati namba 8 hadi 11 za Bandari ya Dar es Salaam,“ alisema Waziri Mbarawa.

Awali, wabunge mbalimbali walichangia michango yao bungeni akiwamo mbunge wa Biharamulo Magharibi, Ezra Chiwelesa, ambaye alisema kuwa ni vyema Watanzania wakaelewa kwamba suala la bandari linahusisha ushindani mkubwa kutoka mataifa mengine, akionya uwezekano wa mataifa hayo kutumia watu kupotosha suala la uwekezaji katika bandari za Tanzania ili bandari zao ziweze kushinda kibishara.

“Sisi tunaowakilisha nchi kwenye Mabunge ya nje, tunajua upinzani tulio nao na wenzetu wa jirani. Ni lazima kama taifa ifike mahali tusimame, hawezi kuja mtu anayeongea lafudhi ya nchi jirani, mnamuita mbobezi na mtaalam” amesema Chiwelesa.

Upande wake, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango amewaondoa hofu Watanzania akisema Serikali ya CCM na wabunge wake siyo wajinga na hawawezi kuleta bomu kwa kukubali kuwasilisha wala kupitisha mkataba wa kuuza bandari wakati wanakwenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu 2025.

Amesema hofu hiyo imeisaidia Serikali na wabunge kujuwa wananchi wanataka nini na amegundua Watanzania wanajua kuwa bandari ni moja ya chanzo kikubwa cha mapato ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles