Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameshiriki katika mdahalo uliohusu “Miundombinu Thabiti ya Dunia Katika Ukuaji wa Uchumi” uliofanyika wakati wa Mkutano wa 17 wa Ushirikiano baina India na Afrika.
Mkutano huo ambao umeratibiwa na Confederation of Indian Industry-Exim Bank Conclave umehusu namna bora ya kuendeleza ushirikiano na fursa za ukuaji wa kiuchumi kati ya India na Afrika.
Wakati wa Mdahalo huo Waziri Aweso ameeleza kuwa Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kujenga miundombinu thabiti katika kuhakikisha inaimarisha uchumi wake.
Baadhi ya miundombinu aliyoeleza ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa miradi ya maji, ujenzi wa barabara pamoja na kuimalisha bandari na viwanja vya ndege.
Amesema jitihada inayochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika ujenzi wa miradi hiyo utasaidia sana katika ukuaji wa uchumi kwa kuwa itarahisisha uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa.
Aidha, ameelezea mchango wa sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali kwa kushirikiana na serikali kwani utarahisisha ukuaji wa uchumi.
Vilevile, ameiomba Serikali ya India kuendelea kuunga mkono jitihada za Tanzania katika ujenzi wa miundombinu katika sekta tofauti. Pia, alizikaribisha Kampuni za India kuja nchini kuwekeza katika sekta mbalimbali ili kuboresha zaidi miundombinu ambayo itasaidia kukuza uchumi wa Tanzania na hususan katika Sekta ya Maji.
Mdahalo huo, pia uliwahusisha, Emile Ouosso waziri wa Viwanda na uwekezaji kutoka Jamhuri ya Congo, Abid Said Mia Waziri wa Maji kutoka Malawi, Sridharan Madhusudhanan, kutoka India, Siding Maiva Bank ya Maendeleo Afrika na Tejaswi Avasarala kutoka Nigeria.