Na Veronica Simba, REA
MIRADI ya umeme vijijini inayoendelea kutekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imechangia kuboresha maisha ya wananchi wa maeneo hayo.
Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam leo Julai 3, 2022 na Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu alipokuwa akizungumza na waandshi wa habari.
Akizungumza katika Banda la REA lililopo kwenye Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa (SabaSaba), Mhandisi Olotu amesema, umeme vijijini umewapatia wananchi fursa ya kufanya kazi mbalimbali za ujasiriamali hivyo kujiongezea kipato.
Amezitaja baadhi ya kazi hizo kuwa ni pamoja na kuchomelea vyuma, saluni za kike na kiume pamoja na mashine za kusaga nafaka.
Aidha, ameongeza kuwa upatikanaji wa umeme vijijini umewezesha kuboresha huduma mbalimbali zitolewazo kwa umma ikiwemo afya na elimu.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhandisi Francis Songela, amesema kwamba REA imejipanga kuhakikisha inafikisha nishati hiyo katika maeneo yote vijijini, awamu kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
Akifafanua, Mhandisi Songela amesema REA inatambua kiu kubwa ya umeme waliyonayo wananchi vijijini, ndiyo maana kazi ya kupeleka nishati hiyo ni endelevu ikilenga kuvifikia vijiji na vitongoji vyote.