Na WINFRIDA MTOI,Mtanzania Digital
KATIBU Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, amekabidhi bendera kwa timu ta Taifa ya Tanzania inayokwenda kushiriki mashindano ya CANA Zone 4, yanayotarajia kufanyika Aprili 14, 2022, Lusaka nchini Zambia.
Hafla ya kuwaaga waogeleaji hao 18, imefanyika jana Aprili 11, kwenye ukumbi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kukabidhi bendera hiyo, Neema amesema anafurahishwa na mambo yanayofanywa na Chama Cha Kuogelea nchini(TSA) kutokana na viongozi wake wanavyojitoa kuhakikisha wanashiriki mashindano mbalimbali.
” Ni mara chache sana kumkuta mtendaji wa baraza kupongeza chama lakini mimi nina ‘confidance’ kupongeza chama cha kuogelea kwa sababu ya jinsi ambavyo tunaona wakifanya mambo yao. Mambo tulikuwa tunashauriana nao tunaona wanayafanikisha.
“Unapoona kuna idadi kubwa ya waogeleaji kama hii inakwenda kushiriki mashindano, inaonesha ni kwa jinsi gani kuna imani kubwa na ushirikiano mkubwa kati ya wazazi na chama au mipango ambayo chama imejiwekea,” ameeleza Neema.
Amesema kutokana na umri mdogo wa waogeleaji hao ambao wanaokwenda kushiriki mashindano kwa kuogelea katika bwawa la viwango, anaamini watakuja kufanikiwa kuiletea Tanzania medali za Kimataifa.
Aidha amewataka waogeleaji hao kwenda kupambana ili kuiwakilisha nchi vizuri na kuongeza viwango vyao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TSA, Imani Alimanya, amesema wanashiriki mashindano hayo wakiwa ni timu alikwa kwa sababu Tanzania ipo kwenye CANA Zone 3.
Amesema mashindano hayo yatakuwa ni maandalizi kuelekea Jumuiya ya Madola na mashindano ya CANA Zone 3 ambayo Tanzania inashiriki.
“Maandalizi tumefanya mazuri japo kwa muda mfupi kwa sababu tulikuwa a waogeleaji 40, lakini tumechuja na kubaki 18 wakianzia umri wa miaka 11-19,” amesema Alimanya.