32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

CCM wahamasishwa kujisajili kielektroniki

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam kimewahamasisha wanachama wake kujisajili kielektroniki na kulipa ada ili wawe na haki ya kuchagua na kuchaguliwa katika uchaguzi wa ndani unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Baadhi ya wanachama wa CCM Kata ya Buyuni wakimsikiliza Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Simon Mwakifamba (hayupo pichani) wakati wa mkutano uliokuwa na lengo la kuwahamasisha wajisajili kielektroniki.

Kulingana na kalenda ya chama hicho kuanzia Machi 26 hadi 31 vifaa vitasambazwa kwenye ngazi ya shina hadi taifa huku uchaguzi ukitarajiwa kuanza Aprili hadi Desemba 12 utakapohitimishwa kwa mkutano mkuu wa taifa.

Akizungumza na wanachama wa chama hicho Kata ya Buyuni, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Simon Mwakifamba, mabadiliko hayo ya mfumo si hiyari bali ni ya lazima kwa kila mwanachama.

“Unaweza ukawa mgombea una kundi kubwa la watu wanakuunga mkono lakini hawana uhalali wa kuwa wajumbe kwa sababu hawajajiunga kwenye mfumo na hawajalipa ada. Tukianza kujadili fomu za wagombea kama hujajisajili hatutashughulika na fomu yako hivyo usije ukapoteza haki yako kwa sababu ya kukiuka kipengele muhimu kama hiki…utaratibu lazima ufuatwe tuache siasa za mazoeya,” amesema Mwakifamba.

Aidha amewasisitiza wanachama kuchagua viongozi wenye sifa ili wakisaidie chama 2024/25 huku akisisitiza kuepuka kuchafuana.

“Ninaomba haki itendeke kwenye vikao vya kujadili wagombea kuna watu wanaumizwa sana wakati wa uchaguzi, wana uwezo, wanakubalika kwenye jamii lakini wanatengenezewa ajali za kisiasa.

“Tusitengenezeane ajali, tusitengenezeane kashfa, tusichafuane. Kipindi hiki ndio kipindi cha nongwa wale wa magumashi waelewe uchaguzi wa mwaka huu utakuwa tofauti tunataka haki itendeke,” amesema.

Naye Katibu wa UWT Mkoa wa Dar es Salaam, Paulina Bupamba, amesema wanatembelea kata mbalimbali kuwahamasisha wanachama kujisajili kielektroniki, kujipanga kwa uchaguzi na sensa ya watu na makazi.

“Sensa ni wajibu wako inaleta maendeleo kwako, muhamasishe mwenzako tulete maendeleo,” amesema Bupamba.

Katibu wa CCM Kata ya Buyuni, Juma Mnambya, amesema walifanya ziara katika matawi yote manane kuelimisha usajili wa kielektroniki na kwamba wanachama 5,592 kati ya 8,000 wamesajiliwa.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Buyuni, Athumani Maembe, amewataka wana – CCM kuacha mazoeya na kulipa ada kwa ustawi wa maendeleo ya chama hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles