23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Madiwani Bariadi wampinga DC, CCM

Na Derick Milton, Bariadi

Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu wameendelea kupinga uamuzi uliofanywa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Lupakisyo Kapange pamoja na Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya kwa kuondoa magari madogo ya abiria (Mchomoko) ndani ya standi kuu (Somanda) hali iliyosababisha halmashauri hiyo kuanza kushuka kwa mapato yake.

Maamuzi hayo ambayo madiwani wameendelea kuyapinga ni kuyaondoa magari madogo yaliyokuwa yakipaki ndani ya stendi hiyo mpya na kuyaruhusu kuendelea kuingia katikati ya mji wa Bariadi na kupaki eneo la soko kuu la Wilaya ilipokuwa stendi ya zamani.

Wamesema kuwa kitendo hicho  kilichofanywa na mkuu huyo wa wilaya naHalmashauri Kuu ya CCM ni kuingilia mamlaka ya halmashauri na kimefanywa kisiasa zaidi bila kuzingatia maslahi mapana ya halmashauri na Serikali.

Katika kikao cha Baraza la Halmashauri kilichofanyika jana Madiwani hao walisema kuwa wameshangazwa sana na maamuzi hayo kwani lengo kuu la kujengwa kwa standi hiyo lilikuwa kuhudumia mabasi makubwa na madogo ya abiria yaendayo nje na ndani ya mkoa wa Simiyu.

Kija Bulenya ni Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo na mjumbe wa kamati ya fedha alisema mapato ya halmashauri yameendelea  kushuka  kwa kasi kutokana na maamuzi yaliyofanyika bila kushirikishwa wao na wataalamu.

“Katika taarifa yetu ya kamati ya fedha tuliyoiwasilisha leo katika kikao cha baraza la madiwani tumeeleza ni namna gani maamuzi ya viongozi wetu yanavyoendelea kuiumiza halmashauri…mapato yetu kwa sasa yameshuka na yataendelea kushuka kama hatutachukua hatua za haraka za kurudisha gari ndogo ndani ya standi kuu… na lengo la kujengewa standi ile ni kukusanya mapato yatakayoisaidia halmashauri kutekeleza miradi ya wananchi,” amesema Bulenya.

Aliongeza kuwa hapo awali kabla ya kuamishwa kwa magari hayo madogo ,halmashauri hiyo ilikuwa ikikusanya kiasi cha Sh milioni 25 hadi Milioni 28 kwa Mwezi, lakini kwa sasa mapato yameshuka sana na kufanya makusanyo kuwa Milioni 15 hadi 13.

Diwani wa kata ya Buhnamala, Samola Nola amesema standi ya somanda imetumia gharama kubwa ya katika ujenzi wake baada ya halmashauri kupata fedha kutoka Benki ya Dunia zaidi ya Bilioni 7 na itashangaza sana kama miundombinu iliyojengwa haitatumika kuipatia mapato halmashauri.

Aliongeza kuwa ifikie wakati tuache siasa katika kutekeleza shughuli za serikali kwa manufaa ya wananchini ambao ndio msingi mkubwa wa mambo yote.

“Tunatambua wazi siasa ni muhimu lakini siasa hiyo isije kuharibu utekelezaji wa mikataba ya wafadhili wetu waliotujengea standi hiyo…na endapo mfadhili atagundua mradi wetu wa stand ya somanda haufanyi vizuri hatutaweza kupata fedha zingine za miradi kama hiyo,”amesema.

Diwani wa kata ya Isanga Nashon Ngusa amesema: “Tunatambua kuwa viongozi wetu waliamua kisiasa bila hata kuturuhusu tutoe maoni yetu na endapo hatutaliangalia jambo hili tutaendelea kushuka kimapato,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Lupakisyo Kapange akizungumza kwenye kikao hicho alitetea uhamuzi ambao walifanya wa kuhamisha magari madogo ndani ya stendi hiyo kuwa ulikuwa sahihi kwani walipata baraka zote kutoka Halmashauri Kuu ya CCM ya wilaya.

“Najua kuna fununuza chini kwa chini za halmashauri kutotaka kufanya marekebisho ya kujaza vifusi eneo la standi ya zamani  ambako tulihamishia gari ndogo kwa sababu ya  maamuzi  tuliyoyafanya  kwa maslahi ya chama.

“Ila niwaagize mtekeleze maagizo hayo na suala la kuhamisha magari… tulikuwa sahihi sana, na wala hatukufanya kwa kukurupuka, tulikuwa sahihi ni vyema mkatekeleza maagizo hayo,” amesema Kapange.

Katibu wa CCM Wilaya ya Bariadi, Masanja Salu aliwataka wajumbe wa baraza hilo kutoendelea kujadili suala hilo kwenye kikao hicho kwa kuwa lilipitia ndani ya Halmashauri Kuu ya CCM wilaya na kwamba warudi tena ndani ya chama ili waweze kujadili na kupata muafaka sahihi.

Mwenyekiti wa halmashauri, Elias Masanja alisema uamuzi huo haukubaliki na madiwani na utaikosesha Halmashauri fursa nyingine ya kupata fedha kutoka banki ya dunia kwa ajili ya maendeleo ya wananachi wao.

————

Awali, iliandikwa Kamati ya Siasa Wilaya ya Bariadi badala ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Bariadi, hivyo tunaomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza.

Mhariri

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles