24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Sh bilioni 4.8 kuboresha huduma Hospitali ya Amana

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana imepatiwa Sh bilioni 4.8 kuboresha huduma kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda Muhimbili na Mloganzila.

Mkakati huo wa Serikali wa kuzijengea uwezo hospitali za rufaa utaiwezesha Amana kutoa huduma ambazo awali hazikuwepo kama za vipimo vya CT Scan na kusafisha damu.

Akizungumza wakati kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Ilala ilipotembelea hospitali hiyo Mganga Mfawidhi, Dk. Bryson Kiwelu, amesema fedha hizo zitatumika kukarabati miundombinu na ununuzi wa vifaa tiba.

Amesema kati ya fedha hizo Sh bilioni 2.6 zitatumika kununua Vipimo vya CT Scan na Digital X- ray na hivyo kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda Muhimbili na Mloganzila kwani wastani wa wagonjwa watano hadi sita hupelekwa kila siku.

Aidha amesema Sh milioni 600 zitatumika kununua vifaa tiba katika kitengo cha wagonjwa wa dharura wakati Sh milioni 700 zitatumika kununua vifaa tiba kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa mahututi na tayari wamepokea vifaa vya Sh milioni 40 kutoka kwa wazabuni mbalimbali.

Kwa mujibu wa Dk. Kiwelu shughuli nyingine ni upanuzi wa kitengo cha magonjwa ya dharura, kitengo cha wagonjwa wa nje na kitengo cha wagonjwa wanaohitaji matibabu ya uangalizi maalumu ambapo wodi moja imepandishwa hadhi inakarabatiwa iwe na mwonekano wa kisasa.

Aidha amesema kitengo hicho kimeunganishwa na huduma ya kusafisha damu na kwamba tayari wameshapokea vifaa vya kusafisha damu na shughuli za ujenzi zinaendelea.

“Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yameongezeka sana na hasa wagonjwa ambao wanahitaji kusafisha damu, gharama imekuwa kubwa na haipatikani kwa urahisi ndio maana hospitali za rufaa zinajengewa uwezo wa kusafisha damu,” amesema Dk. Kiwelu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, amesema wanakagua miradi inayotekelezwa katika kata mbalimbali ili kujiridhisha ubora na thamani ya fedha inayotumika.

“Tunapita kukagua miradi mbalimbali ambayo mheshimiwa rais ametoa fedha na ambayo inaigusa jamii moja kwa moja ili kuhakisha tunakuwa na majengo mazuri na yanayolingana na thamani ya fedha,” amesema Ludigija.

Kamati hiyo pia ilikagua mradi wa majitaka unaotekelezwa katika Kata za Vingunguti na Mnyamani ambao umewanufaisha wananchi 310 wanaoishi katika mazingira duni waliotengenezewa mfumo rafiki wa kuzoa majitaka.

Miradi mingine iliyokaguliwa ni Vituo vya Afya Kiwalani, Kinyerezi na Segerea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles