27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

RC Mtaka anusa ubadhilifu ujenzi wa Hospitali

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amesimamisha shughuli za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kondoa (Bukulu) kutokana na kunusa harufu ya ubadhilifu, uzembe na ukosefu wa mafundi.

Aidha, ameagiza wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuusimamia mradi huo kuanzia Jumanne ya wiki ijayo.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, akielekea katika eneo la ukaguzi huo.

Akizungumza Januari 28, 2022 katika eneo ambalo inajengwa Hospitali hiyo la Bukulu, wilayani Kondoa baada ya kupokea taarifa ya ujenzi wake, Mtaka ameagiza kusimamishwa kwa ujenzi huo kutokana na kutokuridhishwa na kasi ya ujenzi.

Katika ziara hiyo, RC Mtaka alikuwa ameongozana na Katibu Tawala wa Mkoa, Dk. Fatma Mganga, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wataalamu kutoka Ofisi ya yake ambapo alipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, DK. Hamis Mkanachi na wataalamu kutoka katika Halmashauri ya Kondoa.

Akizungumza kwa masikitiko Mkuu huyo wa Mkoa amesema haiwezekani mradi mkubwa kama huo ambao Serikali imetoa Sh bilioni 1.8 halafu fundi awe mmoja na vifaa vichelewe kufika.

“Naagiza shughuli za ujenzi zisimame kuanzia Januari 28, zitaanza Februari 2, baada ya timu ya wataalamu kutoka mkoani wakiongozwa na Mhandisi Happiness Mgalula na Aziza Mumba hapa kabla ya kuanza kwa ujenzi watakagua kila kitu na watu kutoka Ofisi ya Rais na TAKUKURU watakuwepo.

“Baada ya uhakiki kuanzia vifaa vilivyopo benki kuna Sh ngapi, haiwezekani kila siku tuwe tunakuja katika mradi ambao hakuna kinachoonekana ni aibu ni aibu kubwa sana mkuu wa wilaya,”amesema Mtaka.

Amesema Halmashauri ya Kondoa kupitia Mkuu wa Wilaya imeonesha udhaifu mkubwa katika kusimamia miradi ikiwemo mradi huo kwa kushindwa kuleta mafundi na vifaa.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, DK. Mganga amesema kilichotokea ni kutojiongeza kwani fedha waliishapewa muda mrefu ambapo amedai wao ni watumishi wanapaswa kujitafakari kwa kilichotokea.

“Tunatoa maagizo kila siku hili jambo halifanyiwi kazi ,hela zote mnazo hakuna mnachofanya mpaka watu wa Mkoani ndio waje nyie hamshtuki mpo tu,”amesema Dk. Maganga.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Dk. Mkanachi amesema kumekuwa na shida hasa ya mawasiliano ambapo amesema changamoto ya shida ya maji wameitatua na wamekaa nao wataalamu hakuna ambaye anasema shida ni nini.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kondoa, Mohammed Kova amesema kuna jambo limejificha kwa ndani hasa baada ya Halmashauri kupelekwa Bukulu.

Amesema haiwekani fedha zikawa zipo lakini utendaji ukawa wa kusua sua hivyo wao kama Chama kuna sehemu ya kuwabana na kuwawajibisha viongozi ambao hawatimizi wajibu wao.

“Fundi wa Kujenga anatoka nje ya Bukulu hapa hakuna mafundi mpaka watoke Mwanza,Tanga hapana hapa kuna kitu na lazima tupendane,tushikamane tuwatumikie wananchi,”amesema.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Dk. Best Magoma amesema wao wanasubiria Hospital hiyo iweze kukamilika ili waanze kutoa huduma.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amefika katika Kijiji cha Bubutole Wilayani Chemba Mkoani Dodoma kujionea daraja ambalo limekatika huku akitoa pole kwa wakazi wa eneo hilo.

Akiwa katika eneo hilo ameipongeza Wakala wa Barabara (TANROD) kwa ujenzi wa daraja la muda. Daraja la Bubutole linaunganisha Mikoa ya Dodoma na Singida.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TANROD Mkoa wa Dodoma, Saleh Juma amesema wameanza kufunga daraja la chuma ambapo amedai mpaka kesho (Jumatatu) magari yataanza kupita.

Amesema kwa sasa wamefunga daraja la mbao ambalo linawasaidia wakazi wa eneo hilo kupita ambapo pia mabasi hupaki upande wa pili na kisha abiria hupita na kupokelewa na basi lingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles