Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
JUMLA ya madereva 537 wamefungiwa leseni zao za udereva katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2021 baada ya kuonekana kuwa sugu kwa kufanya makosa hatarishi barabarani.
Madereva 472 wamefikishwa mahakamani, huku 107,146 wamelipishwa faini za hapo kwa hapo, wakati 1,720 wakipewa onyo.
Hayo yamesemwa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, SACP Wilbroad Mutafungwa mbele ya Rais Samia Suluhu Hassani wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Nenda kwa Usalama leo Novemba 23,2021 mkoani Arusha.
SACP Mutafungwa amesema hatua hizo ni katika usimamizi wa kisheria na kanuni kwa madereva kwa kuzingatia makosa hatarishi yanayosababisha madhara makubwa kama kuendesha huku dereva anaongea na simu, ulevi na mwendokasi, kutofunga mkanda na ukosefu wa viti vya kuwalinda watoto ndani ya gari.
Hata hivyo amesema hali ya usalama barabarani inazidi kuimarika kutokana na ajali za barabarani kuendelea kupungua.
Akitoa takwimu za matukio ya ajali za barabarani za kipindi cha miaka minne iliyopita, amesema hali hiyo pia imechangiwa na uotoaji wa elimu kwa njia mbalimbali ikiwamo vipindi vya redio na runinga.
Ametoa takwimu za ajali zinazoanzia Januari hadi Septemba kwa kila mwaka kuwa “Mwaka 2018 jumla ajali zilikuwa 3,732, mwaka 2019 ajali ni 2,704, hivyo tumefanikiwa kupunguza matukio ya ajali 1,028 sawa na asilimia 27.5.
“Vifo vilivyotokana na ajali katika kipindi hicho, ni mwaka 2018 vifo ni 1,788 na mwaka 2019 ni 1,440, hivyo tumepunguza vifo 348 sawa na asilimia 19.5.
“Majeruhi mwaka 2018 walikuwa 3,746, mwaka 2019 majeruhi 2,830, hivyo tumefanikiwa kupunguza majerhi 912 sawa na asilimia 24.3.
“Mwaka 2019/2020 ulinganisho, matukio ya ajali yalikuwa 2,704, mwaka 2020, 1,714, hivyo tukawa tumefanikiwa kupunguza matukio 990 sawa na asilimia 36.6. Mwaka 2019 vifo vilikuwa 1,440 mwaka 2020 , vifo 1,270, kukawa na punguzo la vifo 170, sawa na asilimia 11.8.
“Majeruhi mwaka 2019 walikuwa 2,830, mwaka 2020 walikuwa 2,126, tumefanikiwa kupunguza 708 sawa na asilimia 25.0.
Katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2020 ajali ni 1,388, mwaka 2021 ajali 1,187, hivyo tumefanikiwa kupunguza ajali 201 sawa na asilimia 14.5.
“Januari hadi Septemba mwaka 2020, vifo vilikuwa 949, 2021 ni vifo 900, tumepunguza vifo 49 sawa na asilimia 5.2.
“Majeruhi mwaka 2020 walikuwa 1, 672, mwaka 2021 katika kipindi hicho, majeruhi 1,405, hivyo tumefanikiwa kupunguza 267 sawa na asilimia 16.0, “
Aidha ametaja baadhi ya sababu za ajali za barabarani kuwa ni pamoja na makosa ya kibinadamu kama vile ni ulevi, mwendokasi, uzembe wa madereva na watembea kwa miguu, pia madereva wa pikipiki kutokuvaa kofia ngumu.
Ameeleza kuwa nyingine ni ubovu wa vyombo vya moto, utelezi, mvua kubwa, ukungu na miundombinu ya barabara.
Pia amemuomba Rais Samia kupatiwa vifaa vya kisasa vya kusaidia kukabiliana na ajali za barabarani ikiwamo vifaa vya kisasa vya ukaguzi wa magari.