24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia awataka askari wasiwe kero barabarani

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

RAIS  Samia Suluhu Hassan  amewataka  askari wa usalama barabarani kujenga urafiki na watu wanaofanya nao kazi kuliko kuwa kero kwao ili kukabiliana na ajali.

Akizungumza leo Novemba 23, 2021 wakati akizindua  maadhimisho ya  Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani,  yanayofanyika  mkoani Arusha, Rais Samia amesema askari wawe msaada ili wananchi wakiwaona wawakimbilie.

“Suala la kusimamia usalama barabarani ni jukumu la Jeshi la Polisi lakini nao sio Malaika, askari wetu wawe na msaada kwa wananchi na sio kero kwa wananchi, wananchi wakiwaona wawakimbilie na sio wawakimbie.

“Kwa sababu ajali nyingine zinatokana na hawa vijana wetu wenye pikipiki, akiona unifomu ziko pale anakata kichochoro, huko anakoenda hajui kuna nini, ajali zinatokea, kwa hiyo askari mjitahidi sana kuwa wenyewe wa usalama barabarani.



Rais wa Samia Suluhu Hassan, akikabidhi jumla ya pikipiki 26 kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP, Simon Sirro kwa ajili ya kuongeza kasi ya kufanya doria kwa Jeshi hilo, kwenye maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama yalioanza leo  Novemba 23,2021 katika Uwanja wa  Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Khamis Hamza Chillo.

“Lakini pia kuna kero ndogongogo zinazolalamikiwa kwa askari wetu kwa mfano suala la kushikilia leseni za madereva kwa muda mrefu au kulazimisha madereva kulipa faini hapo hapo wakati  sheria inampa muda dereva kwenda kulipa faini lakini wanang’ana ilipwe hapo hapo unajiuliza kuna nini.

“Jingine  ni kwamba kuna ukamataji  mwingi  wa vyombo, ukipita  vituo vya polisi kuna pikipiki nyingi zimepangwa na nyingine haizonekanani kama zimekamatwa jana na leo na utajiuliza kwa nini hizi pikipiki haiondoki pale.

“Kwa sababu kama ni ushahidi wa makosa, makosa yasikilizwe kesi imalizike, hakumumiwe mkosa alafu kazi iendelee.

“Lakini vyombo vinabaki muda na muda, vingine unahisi kama vimetelekezwa na wenyewe, nadhani inagaliwe kwa undani kero hizi  ndogondogo zinasababishwa na nini,” ameeleza Rais Samia.

Aidha  amesema  takwimu zinaonyesha  kuwa waendesha pikipiki maarufu bodaboda bado wamekuwa kinara  wa  kusababisha ajali ambapo  kwa  miaka mitano wapanda  bodaboda 2,220 wamepoteza maisha kutokana na ajali za barabarani, huku majeruhi wakiwa 4,202.


Rais Samia Suluhu Hassan, akipata maelezo kuhusu matumizi ya barabara na madaraja pamoja na kuvuka katika maeneo hayo  kutoa kwa watoto wa shule mbalimbali mkoani  Arusha alipotembelea mabanda ya maonesho kwenye maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yaliyofanyika leo  Novemba 23,  2021 katika Uwanja wa  Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. wa pili kulia Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro.

“Hii ni kusema kwamba kwa mwaka mmoja ndani ya kipindi hiki , tumepoteza vijana 445, waendesha bodaboda peke yao na Mahospitali yetu yalikuwa na vijana 850 kila mwaka wanaotokana na ajali za bodaboda au wao kugonga wengine au  kusababisha gari liue kwa sababu yao.

“Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania mnaondesha bodaboda, kuwa kinara katika takwimu hizi si sifa njema, niombe sana Jeshi la Polisi mnapoendesha elimu ya usalama barabarani mara nyingi bakini na watu wa bodaboda,” amesema Rais Samia.

Amewataja wengine waliochangia  ajali  katika kipindi cha miezi ni madereva wa magari binafsi.

Kutokana na hali hiyo, Rais amelitaka Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani kuzidi kutoa elimu kwa vijana waendesha bodaboda.

Aidha amelitaka jeshi hilo kutumia mitandao ya kijamii kutoa elimu hiyo, pamoja na kuwekeza katika utafiti ili kupata suluhisho la kisayansi la kupunguza ajali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles