Asifiwe George na Amani Makala (RCT), Dar es Salaam
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limeandaa oparesheni maalum ya kuwakamata vijana wanaotumia dawa za kulevya maarufu kama ‘mateja’ na wale wanaozurura ovyo mitaani.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Kamishna, Simon Sirro alisema oparesheni hiyo itawahusisha wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya hususan wale wanaojidunga sindano.
Alisema kila mtu atakayekamatwa akiwa ametumia dawa za kulevya atahojiwa na polisi ataje anakozipata.
“Watumiaji na wauzaji wa dawa za kulevya wanafahamika, wapo wanaopita bandarini na wanaopita nchi kavu lakini tunataka tuwakamate na vithibitisho ili tunapowafikisha mahakamani tunakuwa na ushahidi.
“Ni lazima tuwasaidie vijana wetu ambao wanataka kuharibikiwa kwa matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu wanapozurura ovyo nchi yetu ndiyo inayopata aibu,” alisema Kamanda Sirro.
Alisema jeshi hilo halitamwonea haya kijana yeyote watakayebainika kuuza au kutumia za kulevya na atachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani .