STAA wa muziki wa Afrobeats nchini Nigeria, Yemi Alade, amesema soko la muziki wa Afrika limetawaliwa na wanaume, jambo ambalo linapaswa kuangaliwa upya kwa kuwapa nafasi wasanii wa kike.
Alade ni mmoja kati ya wanamuziki wa kike wanaofanya vizuri, ambapo video za nyimbo zake, ikiwamo ya ‘Johnny’, zimewavutia mamilioni ya watu, achilia mbali kufanya kazi na mastaa wa Marekani, akiwamo Beyonce.
“Nataka kila msanii wa kike aliyeamua kuingia kwenye soko la muziki wa Afrobeats aendelee kupambana. Sidhani tunapaswa kurudi nyuma kwa sababu tu muziki unatawaliwa na wanaume,” amesema Alade.
Bibiye huyo anatamba na albamu zake tano zilizotikisa Afrika na nje ya Bara hili, na hapo unazizungumzia ‘King of Queens’, ‘Mama Africa’, ‘Black Magic’, ‘Woman of Steel’, na ‘Empress’ aliyoachia mwaka jana.