26.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

RC MAKALLA AFANYA MAAMUZI MAGUMU

Na ELIUD NGONDO

-CHUNYA

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, ameyarejesha maeneo ya wananchi waliochomewa nyumba zao na Jeshi la Polisi kwa amri ya Mkuu wa wilaya hiyo, Rehema Madusa, wakidaiwa kuishi kwenye hifadhi ya msitu.

Wananchi hao ni wa kutoka vijiji vya Shoga, Mapalaji B na Ikama vilivyopo Kata ya Sangambi wilayani Chunya.

Uamuzi wa kuwarejeshea wananchi hao zaidi ya 1300, ulitangazwa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo, baada ya tume aliyoiunda kuchunguza sakata hilo kubaini kuwa wananchi hao walionewa.

Makalla alisema wananchi hao walikuwa hawapo kwenye hifadhi na badala yake walikuwa kwenye eneo la msitu wa kijiji na kwamba walipewa maeneo hayo na uongozi wa kijiji na kupatiwa hati za kimila ambazo ziliidhinishwa na uongozi wa wilaya hiyo.

Mkuu huyo wa mkoa alisema vijiji hivyo vilikuwa na viongozi ambao walichaguliwa na wanatambuliwa na Serikali, hivyo operesheni hiyo ilikuwa haina sababu ya kufanyika bila kuwashirikisha.

“Kuanzia sasa wananchi wote mlioondolewa kwenye maeneo yenu mnarejea na mnatakiwa kuendelea na shughuli zenu kama kawaida, nawaagiza viongozi wa vijiji kwa kushirikiana na maofisa wa halmashauri, muwaandalie wananchi hawa matumizi bora ya ardhi,” alisema Makalla.

Alisema kazi ya mkuu wa mkoa na wilaya ni kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na utulivu, wanafuata sheria na kushiriki shughuli za maendeleo.

Makalla alisema wananchi hao waliwatuma wawakilishi wao kusafiri umbali wa zaidi ya kilimita 100 kwenda kuwasilisha malalamiko kwenye dawati lake, madiwani walilalamika na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ulimuomba asaidie kumaliza sakata hilo.

Baadhi ya wananchi hao walidai kuwa waliondolewa kinyama kwenye maeneo hayo kwa kuchomewa mali zao ikiwemo vyakula pamoja na kusachiwa kila walichokuwa nacho.

Mmoja wa wananchi hao, Edson Mliliti, alisema wakati wa sakata hilo zaidi ya nyumba 300 zilichomwa na kwamba hawakuruhusiwa kutoa chochote ndani ya nyumba hizo.

Mliliti alisema askari waliokuwa wanatekeleza operesheni hiyo walikuwa wanapekua mabegi yao na fedha walizozikuta walikuwa wanazichukua na kuondoka nazo.

“Mkuu wa wilaya alifanya kazi hiyo kwa kufuata sheria, lakini sisi tulikuwa hatupo kwenye eneo la hifadhi, hivyo unyama tuliofanyiwa ulikuwa si wa kawaida, vyakula vyetu viliteketea na hatukuwa na namna ya kuvinusuru,” alisema Mliliti.

Diwani wa Kata ya Sangambi ambako vijiji hivyo vinapatikana, Njunjuru Mhewa (CCM), aliishukuru Serikali kuwarejesha wananchi wake akidai kuwa waliondolewa kinyama bila makosa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles