Arodia
Peter, Dodoma
Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo jijini Dodoma, imefanikiwa kupandikiza figo kwa wagonjwa nane kwa kipindi cha miaka miwili tangu kuanzishwa kwake.
Hayo yalisemwa na daktari bingwa wa figo hospitalini hapo Dk. Kessy Shija, jana Mei 4, alipokuwa akiongea na waandishi wa habari waliokuwa kwenye ziara ya kutembelea miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoani humo.
Dk. Shija alisema kuanzishwa kwa huduma hiyo ya kibingwa hospitalini hapo kumepunguza gharama kwa wagonjwa kwenda kupata matibabu hayo nje ya nchi, hususani India.
“Niwashauri Watanzania kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, kwa sababu magonjwa ya kudumu kama figo yanachukua wastani wa Sh, 200,000 hadi 250,000 kwa wiki ambazo ni gharama za kusafishwa, ambapo kwa matibabu ya kupandikizwa figo huchukua wastani wa hadi Sh, 6, 000, 000 kwa mgonjwa mmoja,” alisema.
Aidha Dk. Shija alisema mbali na figo, hospitali hiyo pia inatoa matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa wa moyo kama ilivyo kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.