26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

JPM utakumbukwa na watanzania ukiwaachia katiba bora

JAVIUSI KAIJAGE

AKIZINDUA kiwanda cha kuchakata mahindi cha Mlale JKT Songea Mkoani Ruvuma Aprili 8 mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli alisema ana imani kuwa aking’atuka watanzania watamkumbuka.        

Rais Magufuli kuamini kuwa watanzania watamkumbuka baada ya kuachia ngazi kwa mujibu wa katiba, ni kutokana na yote mazuri anayowafanyia wananchi kwa kipindi kifupi tangu aingie madarakani mwaka 2015.       

Kampeni ya Tanzania ya viwanda na ujenzi wa miundombinu hususan  barabara na reli ni miongoni mwa mambo ambayo JPM amekuwa akijipigia upatu kila mara huku akionyesha viashiria vya kutoridhika na usimamizi wa tawala zilizopita baada ya Mwalimu Julius Nyerere  kwani hapo nyuma viwanda vilikuwepo vingi lakini vikaishia mikononi mwa wajanja.        

Ni dhahiri yote anayoyazungumzia Rais yana mantiki lakini anatakiwa kuelewa chanzo kilichopelekea viwanda na mali nyingine ambazo zilikuwepo katika kipindi cha uongozi wa Mwalimu kuanza kuharibika haraka katika awamu zilizofuata.          

Bila ya kumeza maneno ni kwamba ukosefu wa katiba imara ilikuwa ni chanzo kikubwa cha viongozi kuboronga katika usimamizi wao.          

Barack Obama wakati ni Rais wa Marekani alipotembelea bara la Afrika kwa mara ya kwanza akiwa nchini Ghana Julai, 11, 2009 alisema ili bara la Afrika lisonge mbele  halihitaji watu imara bali taasisi imara.          

Taasisi imara zinajengwa na katiba bora inayoipa Bunge kuwa mhimili wa dola wenye uwezo wa kuuliza, kukosoa, kuhoji na kutunga sheria zenye masilahi mapana ya taifa  bila woga wa kuingiliwa na mhimili mwingine au mihemuko ya kisiasa.        

Katiba bora itazaa taasisi imara  ya Mahakama yenye nguvu  ya kutafsiri sheria  ili  kutoa haki katika mazingira  yaliyo sawa bila kuingiliwa na pande nyingine zenye masilahi binafsi.         

Katiba bora itatoa taasisi imara za vyombo vya habari vitakavyokuwa na uwezo wa kutoa taarifa za ukweli, kufundisha, kuburudisha, kutafsiri  na wakati mwingine kukosoa  bila hofu ya kuingiliwa na  tabaka tawala.          

Katiba bora ni mama wa taasisi imara za ulinzi zisizo na sura ya kutenda mambo yake  kisiasa hususan Jeshi la Polisi lenye majukumu ya kusimamia usalama wa raia na mali zao.        

Watu imara ni wazuri lakini ikumbukwe kuwa na wao ni binadamu ambao mwisho wa siku wanaweza kupatwa na mauti au kustaafu kwa mujibu wa sheria hivyo  kama hakuna katiba imara  wale  wanaoachiwa  madaraka  wanaweza wasisimamie  mambo mazuri  yaliyoasisiwa na watangulizi wao.        

Hayati baba wa taifa, Mwalimu Nyerere alikuwa mtu imara aliyesimamia maadili, akajenga viwanda vingi lakini kwa kuwa hakujenga katiba bora yenye taasisi imara zenye uwezo wa kuendelea kuwasimamia watawala wanaofuata ili wasitoke kwenye ramani, ndiyo maana alipong’atuka mambo yalianza kwenda mrama.        

Marekani imeendelea kuwa taifa kubwa Kiuchumi, Kisiasa na Kijeshi kwa muda mrefu kutokana na katiba bora yenye taasisi imara na ndiyo maana Donald Trump Rais wa sasa pamaoja na ubabe wake wa kutaka kuwa juu ya sheria lakini ameweza kudhibitiwa ilivyo.       

Si tu ukosefu wa katiba bora unaweza kupelekea kushindwa kuendeleza yaliyoanzishwa bali pia inaweza kupelekea kuzaa viongozi madikteta/mafashisti ambao wanaweza kutumia bunge, mahakama, vyombo vya habari  na vyombo vya ulinzi na usalama ili  kuendeleza ukandamizaji wao.        

 Je Tanzania yetu yenye ndoto ya viwanda,  inayo katiba bora yenye taasisi imara kwa maana ya Bunge, Mahakama, Vyombo vya habari na vyombo vya ulinzi na usalama visivyo na mrengo wa kisiasa?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles