Na ELIZABETH HOMBO
-DAR ES SALAAM
FAMILIA ya Baba wa Taifa imezungumzia afya ya Mama Maria Nyerere aliyeugua ghafla akiwa Kampala nchini Uganda kabla juzi kuwasili nchini na kulazwa.
Akizungumza na MTANZANIA jana, msemaji wa familia hiyo, Makongoro Nyerere, alisema mama yake aliugua ghafla akiwa Kampala na baadaye alipowasili nchini alipumzishwa.
Alisema alipelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa afya muda mfupi baada ya kuwasili Dar es Salaam, akitokea Kampala alikokuwa amelazwa baada ya kuugua ghafla.
“Sukari ya mama ilipanda ghafla na kulazimika kupelekwa hospitali ambako baada ya uchunguzi madaktari walimruhusu asafiri kuja Dar es Salaam baada ya afya yake kuimarika kidogo.
“Alipowasili nchini alipumzishwa kwa muda wakati madaktari wakiendelea na uchunguzi kabla ya kufikia uamuzi wa kumlaza… lakini tunamshukuru Mungu anaendelea vizuri,” alisema Makongoro.
Mke huyo wa Mwalimu Nyerere, alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe ya ibada maalumu ya kumbukumbu ya mashahidi wa Uganda eneo la Namugongo iliyofanyika Juni 3, mwaka huu.
Baada ya mjane huyo wa Baba wa Taifa kuugua, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alishindwa kuhudhuria sherehe hizo na kwenda kumtembelea hospitalini.
Kwa mujibu wa BBC Swahili, Museveni alimtuma mwakilishi katika tukio la siku ya mashahidi wa Uganda ili kuwaepusha waumini kusubiri kwa muda mrefu.
Taarifa zilieleza kuwa Mama Nyerere alisindikizwa hadi Uwanja wa Ndege wa Entebbe kupanda ndege ya kurudi nchini kwa matibabu zaidi.
“Mama Maria aliondoka uwanjani humo kwa ndege maalumu iliyotolewa na Rais Museveni, kuelekea jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi,” ilisema taarifa hiyo.
Tangu mwaka 2009, waumini wa Kanisa Katoliki wamekuwa wakifanya ibada katika hekalu la Namugongo kumkumbuka Mwalimu Nyerere.
Juni Mosi, Museveni na Mama Maria Nyerere walishiriki pamoja ibada hiyo maalumu iliyofanyika katika hekalu la mashahidi wa Uganda la Namugongo.
Nyerere alitoa mchango mkubwa kumsaidia Museveni kuung’oa madarakani utawala wa Rais Idi Amin.
Mama Maria amekuwa akisafiri kwenda hadi Namugongo Uganda kwa miaka 13 mfululizo kwa ajili ya sherehe za kuwakumbuka mashahidi wa Uganda.