25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Askari hawa wa TFS wachukuliwe hatua

LEO tumechapisha habari kuhusu wananchi watano  wa Kijiji cha Ikongwe, Kata ya Sitalike wilayani Mpanda wamelazwa baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa risasi sehemu mbalimbali za miili yao na askari wa Wakala wa Hifadhi za Misitu Tanzania (TFS).

Tukio hilo baya limetokea juzi, baada ya askari hao wakiwa na silaha kwenda kuvamia mashamba ya wananchi kuanza kufyeka mazao yao ambayo yalikuwa yamebakiza mwezi mmoja yakomae.

Kitendo cha askari kufyeka mazao bila kupata baraka za mamlaka husika  hakikubaliki kutokana na ukweli kuwa wananchi wengi wanategemea mazao hayo ili kuendesha maisha yao ya kila siku.

Tukio hili linaonekana kuwakwaza wananchi wengi, akiwamo Diwani wa Kata ya Sitalike,  Adamu  Chelehani  ambaye anasema uamuzi wa askari hawa si wa busara kwa sababu walipaswa kuzungumza na wahusika kwanza kabla ya kuchukua hatua.

Anasema kitendo cha askari kutumia nguvu kubwa kiasi hicho wakati wananchi hawajafanya fujo yoyote, kinaonyesha wazi namna ambavyo mamlaka hizi zinaweza kuleta maafa makubwa kwa jamii.

Anasema siku ya tukio hilo, wananchi walifika kwenye mashamba yao baada ya kupokea taarifa ya kuwapo askari hao, lakini hawakufanya fujo yoyote walikuwa watulivu na kuwaangalia askari hao wakiendelea kufyeka mazao yao.

Lakini katika hali ya kusikitisha askari hao walipoamua kupanda gari  lao aina ya Toyota Land Cruiser walianza kufyatua risasi ovyo bila kujali mtu aliyeko mbele yao na kujikuta wakijeruhi watu vibaya.

Katika tukio hili ndugu wanne wa familia moja wamejeruhiwa vibaya  kwa risasi wakati wakiwakimbia askari hawa ambao  kwa kweli wanaonekana wazi kukiuka miiko ya utaratibu wao wa kazi.

Ndugu wanne waliojeruhiwa ni Josephat  Patrick, Jofrey Patrick (39), Fiberiti Patrick (40) na  Januari  Patrick (22) na mwanakiji mwingine Nkuba  Sai aliyepigwa risasi mkono wa kushoto .

Tunapatwa na wasiwasi mkubwa na kujiuliza kama askari hawa nani aliyewapa maelekezo ya kwenda kufanya unyama wa aina hii?

Na kama yupo basi anapaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu. Tunasema hivyo kwa sababu inawezekana kweli tatizo likawapo la wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi za taifa, lakini mamlaka husika zilikuwa wapi tangu wananchi hawa wanaandaa mashamba, wanalima hadi mazao yanaelekea kukoma.

Kama wangekuwa makini kiasi hicho, askari hawa na wakubwa wao wangechukua hatua za kuwazuia tangu wananchi wanaanza kuandaa mashamba kuliko kuwatia umasikini mkubwa hivi.

Kama tulivyosema hapo juu, wananchi wengi vijijini wanategemea mazao hayo kuendesha maisha yao ya kila siku, kusomesha watoto na mambo mengi sasa inakuwaje waharibiwe mazao kiasi hiki?

Inatia uchungu mno kuona mahindi yaliyobakiza mwezi mmoja kuvunwa, yanafyeka na watu wasioheshimu kazi yao, kwani wangeeacha wananchi wakavuna mahidi haya kisha wakafukuza wangepata hasara gani.

Ndiyo maana hata Mbunge wa Nsimbo, Richard  Mbogo (CCM)  ambaye wapiga kura wake wamejeruhiwa, anasema hakukuwa na sababu ya kutumia nguvu kubwa kiasi hicho.

Sisi MTANZANIA, tunalishauri Jeshi la Polisi mkoani Katavi kuwachukulia hatua askari wote waliohusika na tukio hili na wale watakaobainika wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria kujibu tuhuma zainazowakabili.

Kwa kufanya hivi kutasaidia kuwakumbusha askari au mamlaka zinazohusika kuwa na tahadhari kabla ya kuchukua uamuzi wa kuumiza Watanzania hawa masikini ambao maisha yao yanategemea kilimo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles