29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto aibua hoja nane kutekwa Mo

Na Mwandishi wetu


ZIKIWA zimepita siku saba tangu kutekwa kwa mfanyabiashara mashuhuri, Mohammed Dewji (Mo), Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe, ameibua hoja nane juu ya tukio hilo lililotikisa vyombo mbalimbali vya habari duniani.

Baadhi ya hoja za Zitto ni pamoja na kuhoji sababu ya polisi kukataa kualika wachunguzi kutoka nje, kuhoji lilipo ganda la risasi iliyofyatuliwa angani kabla watekaji kuondoka eneo la tukio.

Pia amedai  polisi wamekuwa wakishughulikia matukio ya utekaji lakini wakifika katikati huzuiliwa.

Kutokana na madai hayo ya Zitto, Gazeti hili lilimtafuta Msemaji wa Polisi nchini, Barnabas Mwakalukwa, ambaye alikataa kuzungumzia madai hayo.

Alisema  msemaji wa mambo hayo ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.

Mtanzania ilipomtafuta Mambosasa  kuzungumzia suala hilo, alipokea simu na kusema kama ni mwandishi hazungumzi lolote kwa kuwa anaendelea na operesheni.

Katika andiko la Zitto alilolitoa jana,  alisema Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, Godbless Lema, alitoa pendekezo kuwa Serikali ya Tanzania iombe msaada wa nje kuongeza juhudi za kumtafuta Mo.

Alisema alishangaa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, kulijibu kuwa Serikali haitafanya hivyo kwa sababu jeshi la polisi lina uwezo na utaalamu wa kutosha kuendelea na uchunguzi.

“Naibu Waziri hayupo sahihi kukataa pendekezo la Waziri Kivuli. Nashauri pendekezo la waziri kivuli lichukuliwe kwa uzito unaostahili.

“Uchunguzi wa kutekwa   Mo unapaswa kuwa nguvu kubwa  kuondoa taswira iliyoanza kujengeka nchini kuwa watu wanaweza kutekwa na hakuna kinachofanyika,” alisema Zitto.

Alisema uchunguzi huru wa kimataifa, utasaidia kurejesha imani ya raia na kuwaondolea hofu kuwa wakati wowote wanaweza kutekwa au hata kushambuliwa.

Alisema matukio ya kupotea kwa Ofisa Utafiti na Sera wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema,  Ben Saanane), Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kibondo, Simon Kanguye, Mwandishi wa Habari wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda na kushambuliwa kwa risasi   Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, yanadhihirisha vikwazo vya polisi kufanya uchunguzi.

Alisema baadhi ya vikwazo hivyo ni vya taasisi, na kwamba alifuatilia kutekwa kwa watu hao na kupigwa risasi kwa Lissu akabaini polisi walifanya uchunguzi wakaishia katikati.

Alisema njia ya polisi kuondokana na lawama wanazorushiwa watu wanapotekwa, ni Serikali iruhusu uchunguzi wa kimataifa kwenye suala la kutekwa  MO.

“Nimeshangazwa sana kuwa (Naibu) waziri wa (Mambo ya Ndani), polisi amekuwa mbele kukataa pendekezo hili.

“Kuna maswali hayana majibu katika uchunguzi wa suala la Mohammed Dewji. Baadhi ya vyombo vya habari vimeanza kuyachambua mambo ambayo baadhi yetu waliyahoji mapema sana.

“Haiwezekani mpaka leo ‘footages’ za camera (zilizo kwenye majengo mbalimbali ya alipotekewa Mo)… hizi hazijachunguzwa na kupata namba za gari zilizotumika kufanya utekaji huu na kisha kutambua umiliki wa gari hizi na kupata njia ya kumfikia MO alipo.

“Jeshi la Polisi linasema kamera za hoteli ya Colosseum zilichezewa, watekaji hawawezi kuchezea kamera za mtaa mzima.  Polisi wakipata msaada wa wenzao kutoka nje wanaweza kupata jawabu ya hili.

“Jambo lingine ni kuwa kuna kauli tata kuhusu utekwaji wa Mohammed. Mwanzoni kabisa polisi walisema kuwa MO alitii kukamatwa hakufanya harakati zozote.

“Hata hivyo, ukweli umeanza kutoka kuwa MO alipambana. Katika kupambana alipiga kelele walinzi wasifungue lango la kutokea Colosseum ndiyo maana watekaji wakapiga risasi juu na kufungua lango wenyewe.

“Vile vile kiatu kimoja cha MO kilidondoka na pia kofia ilidondoka. MO katika kuona anazidiwa alidondosha funguo ya gari yake na simu, naamini kuwa alidondosha funguo ya gari makusudi  watu wachukue gari kukimbiza watekaji.

“Bahati mbaya hapakuwa na mtu aliyethubutu kuwakimbiza watekaji wale. Kwa nini hizi taarifa hazikutolewa kwenye press (mazungumzo na waandishi wa habari) ya Mkuu wa Mkoa wa ZPC? Kwa nini umma uliambiwa kuwa MO alikubali tu kubebwa?” alihoji.

Alisema,  “jambo la mwisho kwa leo ni la kawaida kwenye mambo ya uchunguzi, ni ganda la risasi ambayo ilitumika. Limeokotwa na polisi? Kinachoitwa ‘ballistic report’ kimetolewa na kusambazwa duniani kwenye kanzidata za watengeneza silaha?

“Hii ingesaidia sana kuweza kujua umiliki wa silaha iliyotumika na kuwa na njia ya kuwapata watekaji na pia kumpata MO. Jeshi la polisi likipata msaada kutoka nje ya nchi linaweza pia kufanikisha hili.

“Mwisho, kumekuwa na kauli za kusema kuwa ‘wanasiasa wasitake umaarufu’ kwenye tukio hili. Hii ni kauli ya ovyo na inapaswa kupuuzwa.

“Mamlaka za Serikali zimejengwa kusimamiana. Waziri Kivuli, Godbless Lema ana wajibu wa kumhoji Waziri wa Mambo ya Ndani bila kuonekana anaingiza siasa,” alisema.

Zitto alisema hakuna kipindi ambacho Serikali imepewa fursa ya kupumua kwenye tukio kama tukio hilo la kutekwa kwa Mohammed Dewji.

“Wanasiasa wa upinzani tulikaa kimya kupisha vyombo kufanya kazi zake. Serikali kuanza kuweweseka   wabunge wanapotimiza wajibu wao kuhoji kunatia shaka kwamba kuna kitu Serikali inaogopa.

“Serikali inaogopa nini? Wanachokiogopa ndiyo kinaogopesha kukaribisha wachunguzi wa kimataifa?”

 

HISTORIA YA MO

Mo ambaye kwa mujibu wa jarida maarudu duniani la Forbes, ni bilionea mwenye umri mdogo zaidi Afrika akiwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni $1.09, alizaliwa mkoani Singida Mei 8 mwaka 1975 akiwa mtoto wa pili kati ya watoto watano wa Gulam Dewji na Zubeda Dewji.

Akiwa na umri wa miaka mitatu, Mo alikwenda mkoani Arusha ambako alianza darasa la kwanza mpaka darasa la saba kabla ya   Dar es Salaam ambako alisoma shule ya Kimataifa Tanganyika (International School of Tanganyika)

Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, alikwenda  Marekani ambako alimaliza elimu ya Chuo Kikuu katika Chuo cha George Town, moja kati ya vyuo vikuu bora   Marekani kilichopo   Washington akichukua masomo ya usimamamizi wa fedha.

Baada ya kuhitimu elimu ya Chuo Kikuu, alipata kazi   Marekani ambako alikuwa akilipwa Dola za Kimarekani 40,000 (Sh milioni 80). Hata hivyo, alikuwa akilazimika kufanya kazi kwa zaidi ya saa 100 kwa wiki.

Kutokana na kutumia muda mwingi   kufanya kazi huku akishindwa kuweka akiba kutokana na gharama za maisha katika jiji la New York, alijikuta akimpigia simu mara kwa mara baba yake akiomba   msaada wa fedha  aweze kuishi. Baba yake alimshauri kurudi nyumbani Tanzania  akimweleza kuwa kuna fursa nyingi.

Aliporejea  Tanzania mwaka 1998 alianza kazi katika kampuni ya baba yake ya Mohamed Enterprises Tanzania Limited (METL) kama mdhibiti wa fedha na baada ya miaka miwili alipanda cheo na kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO).

Wakati akianza kazi mauzo ya kampuni yalikuwa dola za Marekani  milioni 30. Kwa uongozi wake mauzo yalipanda kwa kiasi kikubwa hadi kufikia dola za Marekani bilioni 1.4 mwaka 2014.

Mo alikuwa nyuma ya kuanzishwa viwanda ambavyo kwa sasa vinafika 24 vikitengeneza  bidhaa kama sabuni, mafuta ya kupikia, vinywaji baridi, nguo, vyakula na nyingine nyingi.

Kutokana na kukua na  kuongezeka shughuli za kampuni, idadi ya wafanyakazi pia iliongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka wafanyakazi 4,000 hadi kufikia wafanyakazi 24,000 kwa sasa.

ldadi ya wafanyakazi walioajiriwa na METL inakadiriwa kuwa  sawa na asilimia nne ya wafanyakazi  katika sekta isiyo rasmi huku kampuni ikichangia asilimia mbili ya Pato la Ndani.

METL pia inafanya kazi katika nchi 10   Afrika ambazo  ni Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Tanzania, Sudan ya Kusini, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Malawi, Zambia na Msumbiji

Lengo la bilionea huyu kijana ni kufikisha mapato ya kampuni Dola za Marekani bilioni tano kufikia mwaka 2020 na kuajiri watu zaidi ya 100,000 katika nchi mbalimbali  Afrika.

 Mo   alitekwa nyara na watu wasiojulikana Alhamisi iliyopita katika Hoteli ya Colosseum, Oysterbay, Dar es Salaam, mahali ambako amekuwa akienda kufanya mazoezi ya mwili (gym).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles