26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, February 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ziara ya Rais Magufuli imetuzindua -Shaka

Na MWANDISHI WETU

-MOROGORO

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro, kimesema ziara ya Mwenyekiti wa wao wa taifa, Rais Dk. John Magufuli katika nchi za Afrika, imetoa mwanga utakaodumisha umoja, ushirikiano na mwendelezo wa historia kabla ya uhuru na mapambano ya Bara la Afrika ambalo hatimaye lilijikomboa katoka kwa wakoloni.

Kauli hiyo ya CCM imekuja siku chache baada ya Rais Magufuli kufanya ziara katika nchi za Malawi, Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe.

Akizungumzia na wazee waasisi wa CCM jana, Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Shaka Hamdu Shaka, alisema kuwa kuna mambo kadhaa watendaji wa chama wamejifunza kupitia ziara hiyo hasa kuhusu masuala ya uongozi.

Alisema ziara hiyo ni ya aina yake kwa mustakabali wa nchi zote zikiwamo za Maziwa Makuu na kusini mwa Afrika kudumisha siasa, uchumi na historia ya bara la Afrika.

Shaka alisema ziara hiyo licha ya kuendeleza dira ya umoja, ushirikiano, udugu, ujirani mwema kwa maendeleo ya kisiasa, kidiplomasia na kiuchumi, itaendeleza misingi kwa mataifa hayo kushikamana zaidi.

Alisema ni ziara ambayo imetanua wigo katika masuala ya elimu, ajira, biashara, utalii na kubadilishana uzoefu, ikisisitiza haja na mipango kazi ya kuendeleza umoja wa Afrika na watu wake wakati wote.

“Wazee wetu waasisi tunawahakikishia CCM Mkoa Morogoro tumejifunza mambo kadhaa. Tutakutana na makundi yote katika jamii.

“Tutafanya hivyo tukijua siasa ni shughuli za makundi. Ikiwa Mwenyekiti wa chama anakwenda Maziwa Makuu kudumisha ujirani na maendeleo, nasi sasa katu hatutajifungia ofisini ila tutakwenda kufanya kazi kwa ajili ya kuhudumia jamii yetu,” alisema Shaka. 

Alisema CCM Mkoa Morogoro itakutana na makundi yote lengo likiwa ni kuendeleza uhusiano, kujitathmini na kujipima iwapo utekekezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM imegusa maisha ya watu kimaendeleo na kutatua changamoto.

“CCM inajali makundi yote ili kubaini utendaji wa Serikali. Kioo kina tabia ya kuona mengi, lakini daima hakijioni. Kioo cha mtu ni mtu. Tutakutana na makundi yote ili kupima ufanisi kwani chama chetu ndicho kimepewa dhamana na wananchi kuongoza watu na kuwaletea maendeleo,” alisema. 

Pamoja na hali hiyo, aliwataka watendaji wa ngazi za chama na jumuiya zake mkoa kwenda kwa wananchi, kusikikiza kero, changamoto na matatizo walionayo hatimaye zishughulikiwe na kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Katibu huyo alisema pamoja na kuwepo ufanisi mkubwa katika maendeleo ya kisekta chini ya awamu ya tano, watendaji wa chama na Serikali hawapaswi kujisahau au kuridhika badala yake wajitume usiku na mchana ili kutimiza malengo yaliyowekwa kupitia ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015/20.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles