Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Zanzibar, Shemata Khamis, amesema Serikali ya Zanzibar imechukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha sekta ya ufugaji wa kuku inakua na kuleta tija kwa wananchi, ikiwemo kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani juu ya mbinu za kisasa za ufugaji bora na udhibiti wa magonjwa.
Khamis alitoa kauli hiyo Oktoba 17, 2024, jijini Dar es Salaam, alipokuwa akihitimisha Mkutano wa Jukwaa la Tasnia ya Kuku na Ndege Wafugwao kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). Alisema kuwa serikali imeimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa ya kuku na ndege wafugwao ili kudhibiti milipuko ya magonjwa na kuimarisha utekelezaji wa afua za afya.
“Mikakati hiyo ni pamoja na kuanzisha mashamba ya kuku, uwekezaji katika maeneo ya kutotoleshea vifaranga vya kuku, kuanzishwa kwa kiwanda kipya cha vyakula vya mifugo, machinjio mapya ya kuku, na maabara za mifugo zinazowezesha uchunguzi na uzalishaji wa chanjo za mifugo. Pia, tumeanzisha vituo vya utafiti wa kuku,” alisema Waziri Khamis.
Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mikakati ya kuhakikisha tasnia ya kuku inakua na kutoa mchango mkubwa katika ajira, uchumi, na kuimarisha usalama wa chakula na lishe.
Khamis aliongeza kuwa serikali inaendelea kutekeleza mikakati ya kuoanisha kanuni na viwango vya ufugaji wa kuku kati ya nchi za SADC, ili kuwezesha biashara za kikanda na kuhakikisha usalama wa mazao ya kuku na bidhaa zake.
“Tumekubaliana kuanzisha programu za pamoja za utafiti kati ya nchi za SADC ili kushughulikia changamoto zinazofanana, zikiwemo udhibiti wa magonjwa na mbinu bora za teknolojia za ufugaji. Pia, tumeanzisha programu za mafunzo kwa wafugaji, madaktari wa mifugo, na wafanyakazi wa ugani, ili kuongeza ujuzi katika usimamizi wa kisasa wa kuku na ustawi wa wanyama,” alieleza.
Waziri Khamis aliwasihi Jumuiya za Kikanda na Kimataifa kuendelea kushirikiana na Tanzania kuboresha tasnia ya kuku na ndege wafugwao, ili kuondoa changamoto zilizopo katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Uboreshaji wa Kijani Tanzania (AGRA), Vianey Rweyendela, alisema kuwa mpango wa kwanza katika nchi za SADC ni kuhakikisha kuna ushirikiano wa maendeleo katika masuala ya kuku na ndege wafugwao.
“Tumekubaliana kuwa na mpango mmoja chini ya SADC ambao utaangazia masuala yote ya kuku na ndege wafugwao. Tumechambua kila nchi ina fursa gani na inapungukiwa wapi, na lengo ni kupunguza uagizaji wa bidhaa za kuku kutoka nje ya SADC,” alisema Rweyendela.
Aliongeza kuwa asilimia 50 ya bidhaa za kuku na kuku wenyewe wanaotumiwa ndani ya nchi za SADC zinatoka nje ya ukanda huo, jambo linalosababisha upotevu wa fedha za kigeni ambazo zingetumika kwa maendeleo mengine.
“Tumeona umuhimu wa kuongeza ustawi wa wakulima kwa kuwasaidia kuongeza tija na faida. Pia, tutaongeza ustawi wa jamii kwa kuongeza kipato kinachotoka nje ya ukanda huu, na hili ni fursa kubwa kwa Tanzania kama mwenyeji wa mkutano huu,” alihitimisha Rweyendela.