28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Zanzibar gizani

maalimNa Bakari Kimwanga, Dar es Salaam

HALI ya kisiasa visiwani Zanzibar sasa ipo gizani baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, kutangaza kuwa suala la kurudiwa uchaguzi si suluhisho na haikubaliki kwani hakuna hoja wala msingi wa kikatiba kufanya hivyo.

Pamoja na hali hiyo, amesema anashangazwa na wajumbe wa Kamati ya Maridhiano, hasa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, kudai kuwa ameagizwa na Rais Dk. John Magufuli kurudia uchaguzi jambo ambalo alidai si kweli.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Maalim Seif alisema moja ya makubaliano ya vikao vya kamati ni pamoja na kutoa taarifa ya pamoja, lakini Balozi Seif na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein wamekiuka na kuanza kusema hadharani mambo ambayo hayajadiliwa katika vikao hivyo.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema pamoja na hali hiyo hadi sasa wamefanikiwa kufanya vikao vinane ambapo cha kwanza kilifanyika Novemba 9, mwaka jana baada ya yeye kumwandikia barua Dk. Shein kuhusu haja ya kukutana na kujadiliana hasa baada ya kufutwa kwa uchaguzi.

 

SHEIN, BALOZI SEIF WAMEBEBA JECHA

Maalim Seif alisema kwamba katika vikao vyote walivyokutana bado Dk. Shein na Balozi Seif wamekuwa waking’ang’ania suala la kurudiwa kwa uchaguzi visiwani humo, huku wakimtetea kwa nguvu zote Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.

Alisema lakini wakati wote yeye amekuwa akisisitiza haja ya kuheshimu maamuzi ya wananchi waliyoyafanya Oktoba 25, mwaka jana katika uchaguzi ambao waangalizi wa ndani na nje na hata Mwenyekiti wa ZEC, walisema ulikuwa huru wa haki na ulifanyika kwa amani na utulivu.

“Rais John Magufuli amefanya kazi kubwa ya kututia moyo ili tukamilishe mazungumzo kwa ufanisi na kwa kuzingatia matakwa ya katiba na sheria. Alikutana na mimi na baadaye Dk. Shein.

“Hata hivyo inasikitisha kwamba hata yeye Rais Magufuli hakuachwa kufitinishwa na wananchi wa Zanzibar, hasa pale Balozi Seif Ali Iddi alipodai hadharani kwamba eti Rais Magufuli katutaka turudi Zanzibar tukamilishe taratibu za kurudia uchaguzi jambo ambalo si kweli na Magufuli hakuniambia nilipokutana naye katika mazungumzo yetu,” alisema Maalim Seif

Alisema kutokana na kutofikiwa mwafaka wa pamoja, walikubaliana kuandaa taarifa ya pamoja ambayo ilielezwa kwamba ingeandaliwa na katibu wa vikao hivyo, lakini sasa ni zaidi ya wiki mbili hakuna kikao kilichoitishwa.

Maalim Seif alisema alilazimika kuandika barua ya kuhimiza kikao cha kupokea taarifa hiyo na kuipitisha, lakini bado Dk. Shein anadai wanahitaji muda.

“Ni wazi kwamba Dk. Ali Mohamed Shein hakuwa na nia njema katika mazungumzo haya na amepoteza sifa ya kuongoza vikao hivyo,” alisema.

 

ABAINI NJAMA

Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia CUF, alisema hivi sasa kuna kile alichodai ni njama za wazi zinazofanywa kwa makusudi na Dk. Shein ya kukwepa kwa makusudi kuitisha kikao cha kupokea taarifa za mazungumzo hayo.

Alisema lengo ni kuhakikisha wanaishinikiza ZEC itangaze tarehe ya uchaguzi wa marudio ili baadaye itolewe hoja kwamba suala hilo limeshaamuliwa.

“Tunazo taarifa za uhakika kwamba ZEC imetakiwa kukutana Januari 14, mwaka huu kwa lengo la kutangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio ambao unatajwa kuwa umepangwa ufanyike Februari 28, mwaka huu. Taarifa hizo zinaeleza lengo la hatua hiyo ni kukwamisha juhudi zinazofanywa na Rais Dk. Magufuli za kutaka kuona ufumbuzi wa haki na unaozingatia matakwa ya kikatiba na kisheria unapatikana.

“Na tukiruhusu hatua hiyo, maana yake ni kuruhusu kikundi cha watu wachache wanaotumia nafasi zao kujifaidisha kibinafsi na bila kujali masilahi mapana ya nchi na watu wake na wasiojali amani na utulivu wa nchi kuitumbukiza katika balaa kubwa sana,” alisema.

Maalim Seif alisema wananchi wa Zanzibar wako taabani na wamekumbwa na fadhaa baada ya kushuhudia maamuzi yao waliyoyafanya Oktoba 25, mwaka jana kupitia uchaguzi huru na wa haki yakiwa yanakanyagwa.

Alisema wananchi wamesubiri kiasi cha kutosha kwa sababu wao viongozi wanajali amani ya nchi ambapo aliwaomba wawe na subira na sasa umefika wakati uvumilivu na subira zao vinafikia kikomo kwa kuhitaji kuona subira zao zinazaa haki.

“Ni vyema tukaweka wazi hapa kwamba kurudiwa kwa uchaguzi si suluhisho na hakukubaliki, kwani hakuna hoja wala msingi wa kikatiba na kisheria wa uchaguzi kurudiwa,” alisema.

 

MGOGORO ULIOPO

Maalim Seif alisema kutokana na hujuma zilizofanywa katika uchaguzi wa Zanzibar mgogoro haukuwa wa lazima na unaweza kutatuliwa kwa haraka kama utakuwapo utashi na utayari wa dhati wa kisiasa na wa kiungozi ambao utazingatia masilahi mapana na endelevu ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kutokana na hali hiyo, ili kulinda misingi ya Katiba ya Zanzibar inayopelekeza utaratibu wa ZEC kufanya maamuzi kama inavyoelekezwa na kifungu cha 119 (1) na (10) ili kujenga uhalali na heshima ya tume hiyo kutekeleza kazi zake, ni lazima mwenyekiti wake Jecha akae pembeni kwa kujiuzulu au kusimamishwa kwani amefanya makosa makubwa.

“Yeye kama mwenyekiti wa tume hakuwa na mamlaka ya kufanya uamuzi wa jambo lolote linalohusu tume bila kupitia vikao halali kinyume cha maelekezo ya wazi wa kifungu cha 119 (10) cha Katiba ya Zanzibar. Akiwa mwenyekiti wa ZEC ametoa tangazo namba 130 katika gazeti la Serikali linalodaiwa kuwa ni uamuzi wa tume la kufuta matokeo ya uchaguzi huku akijua kwamba ZEC haikuwa na kikao Oktoba 28, mwaka jana kupitisha uamuzi huo.

“Akiwa mwenyekiti wa ZEC ametoa tangazo la kufuta uchaguzi huku akijua kwamba hana mamlaka ya kufanya hivyo na akijua kwamba hata tume yenyewe haina mamlaka hayo. Pia amesema uongo hadharani ili kuhalalisha kitendo chake cha kutoa tamko la kufuta uchaguzi kama alivyokiri mwenyewe katika kikao cha tume Novemba Mosi mwaka jana,” alisema Maalim Seif.

 

JECHA NA LUNDO LA VISINGIZIO

Maalim Seif alisema kabla ya mwenyekiti wa ZEC kutoa tamko lake alilodai ni la peke yake la kufuta uchaguzi, alionyesha dhahiri kuwa alikuwa ana ajenda ya siri, ikiwamo ya kuchelewasha kwa makusudi kazi ya kujumuisha matokeo kwa visingizio mbalimbali ikiwamo kuchelewa kufika kwenye kituo cha majumuisho kilichokuwa Hoteli ya Bwawani.

Alisema pamoja na hali hiyo, pia alisingizia anaumwa  ambapo aliondoka mapema wakati kazi hiyo ikiwa inaendelea.

“Kwa mfano Oktoba 27, mwaka jana aliahirisha zoezi hilo kwa madai kuwa ana tatizo la shinikizo la damu. Siku ya Oktoba 28, ambayo kwa mujibu wa sheria ndiyo ilikuwa ya mwisho kutangaza matokeo, mwenyekiti huyo wa ZEC hakuonekana kabisa katika kituo cha kutangaza matokeo.

“Wajumbe waliobaki waliamua kwamba Makamu Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Abdulhakim Ameir Issa aendelee kuongoza tume kukamilisha kazi ya kutangaza matokeo ya urais kwa vile kifungu cha 119 (10) cha Katiba ya Zanzibar kinaruhusu kufanya hivyo na wakati zoezi hilo linaendelea mambo matatu yalijitokeza.

“Kituo cha Bwawani kilizingirwa na Jeshi la Ulinzi la Tanzania (JWTZ) wakitoa amri ya kuzuia kila aliyekuwemo ndani asitoke na aliyekuwa nje asiingie katika eneo hilo.

“Makamu Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Abdulhakim Ameir Issa alipewa taarifa ya wito muhimu na mmoja wa watumishi wa tume na alipotoka nje ya ukumbi wa kikao alichukuliwa na askari polisi na kupekelekwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Kilimani pamoja na luninga ya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na redio ya shirika hilo yalitoa matangazo ya mwenyekiti wa ZEC kufuta matokeo,” alisema.

 

MABALOZI WATUMA UJUMBE

Katika mkutano huo wa Maalim Seif na wanahabari, MTANZANIA iliwashuhudia baadhi ya maofisa ubalozi  ukumbini hapo wakifuatilia hotuba ya kiongozi huyo.

Waliokuwapo ni pamoja na maofisa ubalozi wa nchi za Umoja wa Ulaya (EU), ambao walikuwa wakiwakilisha mabalozi wa nchi hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles