25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Zaidi ya 300 wajitokeza kupima homa ya ini bure Muhimbili

AVELINE KITOMARY – DAR ES SALAAM

ZAIDI ya watu 300 wamejitokeza kupima ugonjwa wa homa ya ini katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kutokana na zoezi hilo kufanyika bure.

 Daktari bingwa wa magonjwa ya ini na mfumo wa chakula, Dk. Tuzo Lyuu aliliambia MTANZANIA Jumamosi jana kuwa katika kuadhimisha wiki ya homa ya ini duniani  ambayo kilele chake ni Julai 28 hospitali imeamua kutoa vipimo bure ili kuhamasisha watu kuendelea kupima zaidi.

“Tunatoa huduma ya vipimo vya ‘hepatitis B’ bure kwa siku ya leo (jana) na tunafanya hivi katika kuadhimisha wiki ya homa ya ini duniani ambapo kilele chake ni Julai 28 na itafanyika kitaifa jijini Dodoma.

“Kwahiyo sisi kama Muhimbili tumeamua kutoa huduma hiyo bure tuna mpango wa kupima wagonjwa 500 lakini hadi sasa waliosajiliwa ni 300 na bado watu wanaendelea kujitokeza,” alisema Dk. Lyuu.

Dk. Lyuu alisema lengo la kufanya hivyo ni kutoa elimu na hamasa kwa watu kujitokeza kupima ugonjwa huo kwani jamii nyingi hazina mwamko kufanya hivyo.

“Zoezi ni la siku moja, hatupimi tu ila pia tunaota elimu kwa watu kuhusu homa ya ini hasa aina ya B (hepatitis B) tunawahamasisha hata wengine wakapime katika vituo vya afya kwahiyo vipimo hivi ni kwa ajili ya kuhamasisha,” alieleza Dk. Lyuu.

Dk. Lyuu amewashauri wananchi kujitokeza kupima homa ya ini hata wasipoona dalili yoyote na kwamba hiyo itawasaidia kupata chanjo hata matibabu ya mapema.

“Ni vizuri kila mmoja akapime kwa sisi madaktari ukimkuta mgonjwa katika hatua ya awali ni rahisi kumsaidia kuliko ukimkuta akiwa na hali mbaya hivyo nawashauri wananchi wakapime kwasababu takwimu zinaonesha madhara ya hepatitis B ni makubwa,”alisema Dk.Lyuu.

Kwa upande wake mmoja wa watu waliojitokeza kupima, Joyce Mushi alisema amepata hamasa kutokana na huduma hiyo kutolewa bure.

“Nilienda hospitali  nyingine nikaambiwa nilipie gharama ya kupima homa ya ini lakini nilivyosikia Muhimbili wanatoa huduma bure nikasema nisipoteze hela niende huko.

“Hapa watu ni wengi sijui kama watamaliza leo ila ingekuwa vizuri waongeze muda wa kupima bure ili watu waendelee kujitokeza,”alisema Mushi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles