25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Fursa kibao Rufiji

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli ameweka jiwe la msingi katika mradi wa kuzalisha umeme wa Rufiji wa Stiegler’s Gorge na kutangaza uamuzi mwingine mpya ambao utatoa fursa nyingi za ajira.

Katika uamuzi huo mpya, Rais  Magufuli ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kukata eneo la ukanda wa juu wa pori la Selous na kuwa Hifadhi ya Taifa na kupewa jina la Nyerere National Park, ikiwa ni kuenzi mchango wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Uamuzi huo ni wazi unatengeneza fursa kama zile za uwekezaji na ajira kwenye hoteli za kitalii, ajira ya madereva wa magari yanayosafirisha watalii, waongozaji wa watalii kwenda kwenye hifadhi hiyo na nyingine.

Kuhusu eneo litakalobaki baada ya kukatwa Hifadhi ya Taifa, Rais Magufuli alisema waachiwe wawindaji kuendelea na shughuli zao.

Akielezea sababu za eneo hilo kubadilishwa na kuwa Hifadhi ya Taifa, alisema ni kuongeza maeneo ya utalii nchini ili kuendelea kukuza pato la taifa kutokana na fedha watakazolipa watalii.

“Kuna siri lazima niwaambie ndugu zangu, kwenye pori la Selous kuna vituo vya uwindaji (hunting block) 47 vimeshachukuliwa, watu wanakuja na ndege hapa wanaua wanyama wanaondoka, bei yake ya chini kwa kituo ni dola za kimarekani 5,000 ambazo ni sawa na Sh milioni 10 kwa mwezi na ukilipa hiyo unaruhusiwa kuua hata nyati 10, kwa ujumla hii Game Reserve’ haitupi faida.

 “Kutokana na hali hii nataka  Game Reserve’ ya Selous tuikate na iwe Hifadhi ya Taifa ili watalii wawe wanakuja hapa badala ya watu kuja kuwinda wanyama wetu,

“Mataifa mengine hawafanyi sana hizi shughuli na uzuri waziri wa Maliasili yuko hapa, huu ndiyo ujumbe wako, kakae kwenye wizara mkapunguze eneo la uwindaji, hilo limesemwa sana lakini utekelezaji umecheleweshwa,” alisema Rais Magufuli.

MRADI

Fursa hizo ni mbali za zile zinazopatikana katika mradi huo alioweka jiwe la msingi  wa Stiegles Gorge ambao Rais Magufuli ametaka upewe  jina la Mwalimu Nyerere kwani hayo yalikuwa mawazo yake na kufanya hivyo ni kumuenzi.

Mradi huo  ambao Rais Magufuli ameutaja kuwa ni mboni ya serikali utakazalisha megawati 2,115 za umeme  na unatekelezwa na Kampuni ya Arab Contractors ya nchini Misri.

Rais Magufuli alisema baada ya mradi huo  utakaogharimu Sh trilioni 6.5, zinazotolewa na Serikali ya Tanzania  kukamilika manufaa yake yatakuwa si tu kwenye nishati bali pia kwenye sekta nyingine za uchumi na uzalishaji.

“Ndugu zangu mradi huu utatufanya tuwe na umeme wa kutosha na wa uhakika, utakaa kwa zaidi ya miaka 60 na bei yake itakuwa chini na kwa tathimini tuliyoifanya vyanzo vingine vingetugharimu.

“Manufaa mengine; kama nilivyogusia mradi huu utakuwa kichocheo kikubwa kwa maendeleo ya sekta ya viwanda, azma hii haiwezi kufikiwa bila kuwa na umeme wa uhakika na wa bei nafuu, ni dhahiri kulingana na bei ya umeme kwa sasa baadhi ya wajasiriamali wanashindwa kuanzisha viwanda.

“Tatu; mradi huu pia utakuza biashara nchini hali kadhalika wawekazaji kutoka ndani na nje kwa sababu hatuwezi kuvutia wawekezaji kwa umeme unaokatika mara kwa mara.

“Nne; mradi huu utasaidia kutunza mazingira si tu katika eneo hili bali nchi nzima kutokana na matumizi ya kuni na mkaa ambapo Dar es Salaam ndio inaongoza kwa kutumia mkaa kwa asilimia 95, hivyo ni wazi kwamba ukikamilika utachangia kuhifadhi misitu yetu na matumizi ya kuni na mkaa yatapungua,”alisema.

Rais Magufuli alirejea kauli kwamba kumekuwapo maneno kuwa mradi huo utaharibu mazingira jambo alilosema halina ukweli. 

“Lakini pia niseme kuhusu suala la uhifadhi hakuna mtu wa kutufundisha kwa sababu Tanzania ni kinara katika kutunza na kuhifadhi mazingira sisi tunaongoza barani Afrika kwa kutenga maeneo ya uhifadhi,”alisisitiza.

Aliwataka wakandarasi wanaosimamia mradi huo kukamilisha ndani ya muda uliopangwa au kabla ya muda huo.

Rais Magufuli pia alitoa maelekezo kwa Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha na Tanesco kuhakiisha bima ya mradi huo kwa asilimia 100 inatolewa na serikali.

Pamekuwa na mabishano kati ya makampuni, sasa natoa maelekezo bima ya mradi huu kwa asilimia 100 lazima itolewe na bima ya serikali (Shirika la Bima Tanzania), kwa hiyo waziri zingatia hili pamoja na Wizara ya Fedha na Tanesco…ole wenu akasaini na mtu mwingine,”alisema.

Pia alilisisitiza kuwa vibali vya wafanyakazi vishughulikiwe mapema kwa sababu wamekuwa wakichukua muda mrefu na kwamba wanaopewa wawe ni watalaamu.

Akizungumzia kuhusu ajira katika mradi huo, aliagiza wananchi wa maeneo yanayozunguka mradi huo wapewe kipaumbele.

“Hawa ndio walilitunza hili pori tangu dunia ilipoanza kama sio baba zao basi watakuwa babu zao,”alisema.

Alisema kupitia mradi huo zitapatikana ajira 6,000, huku akiwataka wale watakaofanikiwa wakawe waaminifu.

“Niwaombe mtakaofanikwa mkawe waaminifu msiibe vifaa, mafuta, misumari, nondo lakini pia mkiiba mtakuwa mnaiibia Serikali na ninyi wenyewe,”alisema.

Vilevile alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukulia mradi huo kama mboni ya Serikali kwa kuusimamia vizuri katika ulinzi.

FEDHA ZA DHAHABU ZAPANGIWA MATUMIZI

Mbali na hilo, Rais Magufuli alisema fedha na dhahabu zilizokamatwa nchini Kenya na kurudishwa nchini juzi, zikatumike kujenga barabara ya lami kutoka lilipo pori la Selous hadi eneo la Fuga inakopita treni ya umeme ya Standard Gauge.

 “Juzi nimepokea dhahabu zilizorudishwa kutoka Kenya nimepiga hesabu vizuri ni kama Sh bilioni nne au tano na fedha taslimu kama milioni 500, nataka hizo fedha zianze kutengeneza barabara ya lami kutoka hapa hadi eneo la Fuga ambazo ni kilometa 60 ili watu wakitoka Dar es Salaam kwa treni wakishuka pale Fuga wanatumia barabara hadi hapa kuja kutalii,”alisema Rais Magufuli.

HOTELI YA DOLA 3,000

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alieleza kushangazwa na gharama inayotozwa na hoteli iliyopo maeneo hayo ambayo chumba kimoja hulipisha dola za kimarekani 3,000.

“Na watu wanakuja na kuondoka huku, sijui kama mawaziri mnajua hizo fedha tunapata asilimia ngapi, wala sijui kama vyombo vya usalama vinajua mali kiasi gani inasafirishwa kutoka hapa,”alihoji Rais Magufuli.

WAZIRI KALEMANI

Awali, Waziri wa Nishati, Medard Kalemani alisema mradi huo ni mkakati wa kupambana na mazingira kwamba  asilimia 71.2 ya Watanzania wanatumia nishati ya kuni na mkaa kutokana na kukosa nishati mbadala ikiwemo umeme.

 “Utasaidia kudhibiti uharibifu wa mazingira maana magunia ya mkaa milioni tano kila mwezi yanatumika na asilimia 71.2 ya watanzania wanatumia nishati mbadala ya mkaa na kuni, takribani ekari 800,000 hukatwa tukiendelea hivi kufikia mwaka 2030 takribani ekari milioni 2.8 zitakatwa kwa ajili ya kupata nishati ya mkaa na kuni,” alisisitiza Kalemani.

Alisema jambo muhimu katika mradi huo ni ujenzi wa bwawa kubwa litakaloweza kuhifadhi maji ya mita za ujazo bilioni 33.2.

Alitaja faida nyingine kuwa ni kujengwa mashine tisa  zitakazozalisha megawati 235 kila moja na hivyo kufanya jumla ya megawati 2,115.

“Tutazalisha kilovoti 400 ni umeme mkubwa utakaowezesha kuzalisha umeme wa kutumika viwandani utakaosafirishwa kwenda Chalinze hadi Dar es Salaam na mwingine hadi Dodoma na ndiyo umeme utakaotumika pia katika treni ya mwendokasi.

“Rais Magufuli ulitoa maelekezo kwamba lazima tupate megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025 mradi huu ni kichocheo kikubwa sana kuelekea kupata megawati hizo, utatosha kuendesha shughuli za viwanda,” alisema Kalemani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles