27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TRA yaokoa bil 1.5 mashine za kamari

KOKU DAVID-DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA) imeokoa sh. bilioni 1.5 ndani ya miezi miwili baada ya kufanikiwa kukamata mashine za bahati nasibu ambazo zimeingizwa nchini bila ya kufuata utaratibu.

Akizungumza jijini Dar es salaam juzi baada ya kukamata mashine hizo, Kaimu Meneja wa Mkoa wa Kodi wa Ilala,  Stephen Kauzeni, alisema katika eneo la Mikocheni Viwandani TRA ilifanikiwa kukamata mashine  250 ikiwa ni mara ya pili baada ya awali kukamata mashine 1000.

Alisema mashine hizo ziliingizwa nchini kama vifaa vitakavyotumika kutengenezea mashine hizo.

Alisema iwapo mashine hizo 250 zingeingia mtaani zingeisababishia serikali upotevu wa kodi sh. milioni 300 kwa mwaka huku zile 1000 zilizokamatwa awali zingeipotezea sh bilioni 1.2.

“Kwa kushirikiana na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha mashine ambazo zinatakiwa kuwepo mtaani zimewekewa alama na kwamba zile ambazo zitakuwa hazijawekewa alama hazitambuliwi,” alisema Kauzeni.

Alisema mmiliki wa mashine hizo ni Imtiaz Abdulaziz Bandari ambaye namba yake ya utambulisho wa mfanyabiashara (TIN) ni mkoani Mbeya lakini taarifa zake zinaonyesha aliacha kufanya biashara tangu mwaka 2014.

Alisema mfanyabiashara huyo jina alilosajilia kibiashara ni Bahati Jackpot na kwamba alishirikiana na kampuni ya China kuingiza mashine hizo kwa makubaliano ya kushirikiana kufanya biashara.

“Mashine hizi zingeipotezea serikali sh milioni 25 kila mwezi ambazo ni sawa na milioni 300 kwa mwaka hivyo sisi kama mamlaka ya mapato mashine hizi tutazizuia kwa kutumia sheria ya ushuru wakati sheria zaidi zikichukuliwa,” alisema Kauzeni.

Alisema zoezi la kusaka wakwepa kodi litakuwa endelevu na kwamba wameshaongea na watu wao wa ushuru kuongeza umakini katika mashine hizo kutokana na kuwa vifaa vinavyotumika katika mashine hizo havina tofauti na vile vinavyotumika katika kompyuta ambavyo ni vigumu kuvibaini pindi mfanyabiashara anapopeleka nyaraka zake.

Naye Meneja Ukaguzi na Udhibiti wa Bodi ya michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Sadiki Elimsu mwagizaji wa mashine hizo hakufuata taratibu wakati wa kuziagiza jambo ambalo ni kosa kisheria.

Alisema mwagizaji wa mashine hizo ni lazima awe na leseni kutoka GBT, awe na cheti kutoka maabara kinachoonyesha mashine hizo kuwa zimepimwa ikiwa ni pamoja na kuwa na viwango vinavyokidhi kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Pia mwagizaji anatakiwa kuonyesha kibali bandarini ili kubaini kama mashine zake zimekaguliwa na GBT pamoja na kuonyesha sehemu ambako zinapelekwa ambako bodi itakwenda kupakagua kama ni sehemu salama na kwamba jukumu letu ni kuhakikisha kama zinafaa au hazifai ikiwa ni pamoja na kuwalinda wateja,”alisema Elimsu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles