26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga yazidi kupeta

YANGA NA MWANDISHI WETU

TIMU ya soka ya Yanga jana iliendeleza kasi ya kuukaribia ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1 ugenini dhidi ya Stand United katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Vinara hao wa Ligi Kuu ambao wameshikilia usukani kwa muda mrefu, wamezidi kuwaacha kwa mbali wapinzani wao Azam FC wanaoshika nafasi ya pili kutokana na michezo 26 waliyocheza, huku Simba ikiendelea kubaki nafasi ya tatu.

Matokeo ya jana yaliiwezesha Yanga kufikisha pointi 68 baada ya kushuka dimbani mara 27 huku wakiwa wamebakiza michezo mitatu kumaliza ligi, ikifuatiwa na Azam iliyojikusanyia pointi 59.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu, sasa wanahitaji matokeo ya ushindi dhidi ya Mbeya City katika mchezo unaofuata na sare moja katika mechi zilizobaki ili waweze kutangazwa rasmi kuwa mabingwa wa msimu huu.

Katika mchezo wa jana, Yanga walianza kucheza kwa kasi na kufanya mashambulizi langoni kwa Stand ambapo walifanikiwa kupata bao la kuongoza katika dakika ya pili kupitia kwa mshambuliaji, Donald Ngoma.

Ngoma ambaye amefikisha mabao 16 msimu huu, alifunga bao hilo la kuongoza baada ya kupiga shuti la mbali akiwa nje ya eneo la hatari ambalo lilimshinda kipa wa Stand na kutinga wavuni.

Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu huku Yanga ikitawala zaidi mchezo, lakini dakika ya 30 walikoswakoswa na Stand baada ya shuti kali lililopigwa na Elius Maguli kupanguliwa na kipa Deogratius Munishi ‘Dida’.

Wakati Stand wakipambana kusaka bao la kusawazisha, Ngoma alitibua mipango yao dakika ya 44 kwa kuandika bao la pili baada ya kuwazidi maarifa mabeki na kumpiga chenga kipa na kuumalizia mpira wavuni.

Dakika 45 za kwanza zilimalizika Yanga ikiongoza kwa mabao 2-0, ambapo kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Amissi Tambwe alifanikiwa kufunga bao la tatu dakika ya 63 kwa kichwa akiunganisha vyema krosi iliyochongwa na kiungo, Simon Msuva.

Tambwe sasa amefikisha mabao 20 na kuongoza katika ninyang’anyiro cha kuwania ufungaji bora msimu huu akifuatiwa na mshambuliaji wa Simba, Hamis Kiiza, aliyefunga 19.

Kipindi cha pili Yanga walifanya mabadiliko ya kuwatoa Kelvin Yondani na Donlad Ngoma na nafasi zao kuchukuliwa na Vincent Bossou na Matheo Antony, huku Stand wakimtoa Frank Hamis na kumwingiza Vitalis Mayanga.

Dakika ya 82 Stand walipata bao la kufutia machozi kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na Maguli baada ya Thabani Kamusoko kufanya madhambi akiwa katika eneo la hatari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles