24 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga yaweka mkakati

Yanga-vs-Etoile-du-Sahel-1-e1429432765972ABDUCADO EMMANUEL NA JENNIFER ULLEMBO, DAR

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa timu ya Yanga chini ya kocha wao, Hans van Pluijm wamewawekea mkakati mzito wapinzani wao Etoile du Sahel ya Tunisia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, lengo ni kuing’oa kwenye michuano hiyo.

Moja ya mkakati huo ni Pluijm kupanga kuwatumia marafiki zake wa Tunisia kuhakikisha anapata taarifa zao za kina ikiwemo kujua udhaifu wao.

Yanga iliyolazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani na Watunisia hao, inatarajia kurudiana nao jijini Sousse Mei Mosi mwaka huu, Wanajangwani hao wanahitaji ushindi wowote au sare ya kuanzia mabao 2-2 ili kusonga mbele kwa hatua ya mwisho ya mtoano.

Pluijm aliliambia MTANZANIA jana kuwa, atawatumia marafiki zake hao kujua udhaifu wao na namna wanavyocheza nyumbani kwani mara nyingi wamekuwa wakifuatilia Ligi Kuu ya Tunisia ‘Ligue 1’.

Mholanzi huyo alisema mchezo huo unahitaji umakini mkubwa bila kukurupuka pamoja na kuwasoma wapinzani juu juu, huku akidai kuwa hakuna linaloshindikana kama wakiamua kupata matokeo wanayoyahitaji ugenini.

“Sipendi kuwaanika rafiki zangu hapa, ila mimi ni mwalimu nafahamika sehemu mbalimbali na kama unavyotambua nilishawahi kufundisha timu Saudi Arabia,” alisema.

Wakati Pluijm akieleza hayo, Etoile wenyewe jana walizidi kuandamwa na mdudu wa sare baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya wapinzani wao Esperance.

Mchezo huo wa Ligue 1 ulishuhudiwa wenyeji hao wakijipatia bao la kuongoza dakika ya 27, lilofungwa kwa njia ya mkwaju wa penalti na Youssef Mouihbi, Esperance nao walipata penalti dakika ya 48 iliyofungwa vema na Haythem Jouini.

Kuivaa Ruvu Shooting leo

Wakati huo huo, Yanga inatarajia kuikaribisha Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Mchezo huo ni muhimu kwa vinara hao wenye pointi 49, ambao kama wakishinda watakuwa wamebakiza mchezo mmoja dhidi ya Polisi Morogoro Jumatatu ijayo, ili kutangaza ubingwa endapo wakiwachakaza na hao.

Kwenye mchezo wa kwanza wa mzunguko wa kwanza timu hizo zilitoka suluhu, Yanga itaingia dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kuifunga Stand United mabao 3-2, huku Ruvu Shooting nayo ikiishinda Mgambo JKT mabao 2-1.

Pluijm aliliambia gazeti hili anajua ugumu wa timu za majeshi, lakini mchezo wa leo ni muhimu sana kwao na amejipanga kuchukua ushindi.

“Mchezo huu ni muhimu sana ukizingatia nipo kwenye mbio za ubingwa, nitamkosa nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Salum Telela wanaoendelea kuuguza majeraha yao, huku pia kiungo Mbuyu Twite mwenye kadi tatu za njano,” alisema.

Yanga ikishinda mchezo huo itafikisha jumla ya pointi 52 na kuwaacha kwa pointi 10 mabingwa watetezi Azam, wanaoshika nafasi ya pili ambao watacheza kesho dhidi ya Stand United.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles