Na Mwandishi Wetu
KIKOSI cha Yanga kimerejea leo Oktoba 20, kutoka Songea na kuungana na mchezaji wao Paul Godfrey ‘Boxer’ kuaga mwili wa baba yake mzazi aliyefariki juzi kwenye hospitali ya Temeke, Dar es Salaam.
Yanga imetua Dar ikitokea Songea katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Majimaji mjini humo na Wanajangwani hao kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
“Kwa niaba ya wanachama, wapenzi na mashabiki wa Yanga, uongozi wa Yanga unatoa pole kwa mchezaji wetu na familia yake yote kwa msiba huu mzito na kwamba klabu iko pamoja naye katika kipindi hiki cha majonzi.
“Mwenyezi Mungu aendelee kumpa nguvu mchezaji wet una familia yake kwa ujumla katika kipindi hiki kigumu,” imeandika Yanga.
Baada ya kumaliza kuaga kikosi hicho kimeelekea moja kwa moja kambini, Avic Town, Kigamboni kujiandaa wa Ligi Kuu dhidi ya Azam utakaopigwa Oktoba 30, 2021 Uwanja wa Benjamin Mkapa.