UONGOZI wa klabu ya Yanga umefanikiwa kukamata tiketi feki za mchezo wao wa marudiano wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Cerce de Joachim ya Mauritius unaochezwa leo katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Tiketi hizo zenye thamani ya Sh 240,000 zilikamatwa baada ya kupewa taarifa za uuzwaji wake katika maeneo ya Manzese na Magomeni, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Murro, alisema baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema juu ya kuuzwa kwa tiketi feki waliamua kufika katika maeneo hayo na kufanikiwa kuzikamata pamoja na watuhumiwa wanne waliowafikisha kwenye vyombo vya sheria.
“Baada ya kupata taarifa hizo tulifika maeneo hayo na kufanikiwa kuwakamata watu hao ambao walikuwa na tiketi hizo mikononi zenye thamani ya Sh 30,000 kila moja huku wengine wakifanikiwa kutukimbia.
“Watuhumiwa hao tumewafikisha katiki vyombo vya usalama huku wengine tukiendelea kufanya msako, lengo ni kuthibiti hali hiyo,” alisema.