27.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 21, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga yagoma kuifuata Simba Zanzibar

katibu+yangaNA JUDITH PETER, DAR ES SALAAM

TIMU ya soka ya Yanga ni kama inawakwepa watani wao wa jadi Simba, baada ya kuachana na mpango wake wa kuweka kambi visiwani Zanzibar kujiandaa na michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoanza Jumamosi hii.

Awali mabingwa hao wa Ligi Kuu walipanga kuifuata Simba Zanzibar, lakini ghafla wamebadili msimamo wao na kuamua kubaki jijini Dar es Salaam kwa madai huenda wakapata tabu ya uwanja wa kufanyia mazoezi wakiwa Zanzibar.

Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha, aliliambia MTANZANIA jana kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kugundua hakuna jipya watakaloibuka nalo kwenye kambi ya Zanzibar ambako timu za Simba na Azam zimeenda kusaka makali ya Ligi Kuu.

“Tumebadili mpango wa kwenda kuweka kambi Zanzibar kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukwepa matatizo yanayoweza kujitokeza ya kukosa uwanja wa kufanyia mazoezi,” alisema.

Alisema Yanga itaanza mazoezi rasmi kesho baada ya nyota wake waliokwenda kuzitumikia timu za taifa kuungana na wenzao ili kuanza mikakati kabambe ya kupambana kwenye ligi hiyo.

Wachezaji hao ni Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ Salum Telela, Deus Kaseke, Simon Msuva walioichezea timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ juzi ambao wanatarajiwa kuungana na wenzao baada ya kambi yao kuvunjwa.

Tiboroha alisema nyota wao wa kulipwa, Vicent Bossou na Thabani Kamusoko, tayari wamerejea nchini tangu juzi na kiungo Haruna Niyonzima na mshambuliaji, Amissi Tambwe, walitarajiwa kutua jana usiku.

Kocha Mkuu wa timu hiyo Mholanzi, Hans van der Pluijm, alikuwa akiwasubiri kwa hamu nyota hao ambao alijivunia kuwa uwepo wao kwenye timu za taifa, unaweza kuleta mafanikio kwenye kikosi hicho kutokana na majukumu waliyokabidhiwa.

Yanga itafungua pazia la Ligi Kuu kwa kuwakaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kuwafunga wapinzani wao hao mabao 8-0 katika mechi ya mzunguko wa pili msimu uliopita.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles