24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga, Simba, Azam zatoa dozi VPL

Pg 32*Kagera, Prisons, Majimaji zabanwa mbavu, African Sports hoi Ligi kuu

NA WAANDISHI WETU

TIMU za soka za Yanga, Simba na Azam jana zilitoa dozi ya vipigo katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara zilizochezwa kwenye viwanja tofauti, huku mabingwa hao watetezi wakiendelea kutamba kileleni mwa ligi hiyo.

Vinara Yanga walijiongezea kasi na kuzidi kujiimarisha kwenye msimamo wa ligi hiyo baada ya kuwazamisha wenyeji wao Mtibwa Sugar kwa mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Simba ambao walipoteza mchezo uliopita dhidi mahasimu wao Yanga, walizinduka na kutoa kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Azam wakicheza nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex, waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union na kuzidi kuwafukuzia wapinzani wao Yanga waliopo kileleni.

Matokeo hayo yamezidi kuzing’arisha Yanga na Azam ambazo zinapigana vikumbo kuwania uongozi kwenye msimamo wa ligi hiyo, huku Simba ikipanda nafasi ya tatu na kuishusha Mtibwa nafasi ya nne.

Yanga wanaongoza ligi hiyo kwa kufikisha pointi 15 baada ya kushinda mechi tano walizocheza sawa na Azam lakini wakitofautiana kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa, huku Simba wakijikusanyia pointi 12 sawa na Mtibwa.

Mtibwa ambao ni wagumu kufungwa na Yanga Uwanja wa Jamhuri, walianza kulishambulia lango la wapinzani wao dakika ya 12 kupitia kwa Shiza Kishuya, lakini shuti alilopiga lilitoka nje na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Yanga walijibu shambulizi hilo dakika ya 13, lakini mshambuliaji, Malimi Busungu hakufanikiwa kuwahi krosi iliyochongwa na Kelvin Yondani na kuokolewa na mabeki.

Bao la kuongoza la Yanga liliwekwa wavuni na mshambuliaji, Busungu dakika ya 53 baada ya kunasa mpira akitumia uzembe uliofanywa na beki wa Mtibwa Sugar, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ wa kuchelewa kuurudisha kwa kipa Said Mohamed.

Timu hizo ziliendelea kushambuliana kipindi cha pili Yanga wakionekana kucharuka zaidi baada ya kupata bao huku kocha Hans van der Pluijm akifanya mabadiliko ya kuwatoa Salum Telela, Amissi Tambwe na kuwaingiza Simon Msuva na Matheo Anthony.

Katika mchezo huo, kocha Mecky Mexime wa Mtibwa alifanya mabadiliko ya kuwatoa Vicent Barnabas, Shiza Kichuya na Mohamed Ibrahim na nafasi zao kuchukuliwa na Ally Shomari, Jaffar Ibrahim na Said Bahanuzi.

Dakika ya 90 mshambuliaji, Donald Ngoma, aliipatia Yanga bao la pili akiunganisha vyema mpira uliotemwa na kipa wa Mtibwa wakati akijaribu kupangua shuti kali lililopigwa na Msuva.

Kwa upande wa Simba wao walianza kucheza kwa utulivu wakionekana kuwasoma zaidi Stand United huku wakifanya mashambulizi hafifu ya kushtukiza langoni kwa wapinzani mara kwa mara.

Dakika ya 17, Jacob Masange wa Stand aliachia shuti kali langoni kwa Simba lakini lilidakwa kiulaini na kipa Peter Manyika kabla ya kiungo Jonas Mkude kujaribu kupiga shuti dakika ya 23 lakini hakuleta madhara yoyote.

Dakika ya 57, Joseph Kimwaga aliyeingia kuchukua nafasi ya Said Ndemla, aliipatia Simba bao pekee na ushindi kwa shuti kali akiunganisha vyema pasi ya Simon Sserunkuma.

Mshambuliaji wa Stand, Elius Maguli, alikosa bao la wazi dakika ya 79 akiwa amebaki na kipa baada ya kushindwa kuunganisha vyema pasi ya Hassan Banda.

Kwa upande wa Azam ambao waliwakaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Azam Complex, walizidi kuhatarisha kibarua cha kocha Mganda, Jackson Mayanga baada ya beki Shomari Kapombe kuandika bao la kwanza dakika ya 47 akimalizia mpira wa kona iliyochongwa na Farid Mussa.

Wakati Coastal wakijiuliza mbinu za kurudisha bao hilo, walijikuta kwenye  wakati mgumu zaidi baada ya mshambuliaji Kipre Tchetche kuifungia timu yake bao la pili dakika ya 75 baada ya kuachia shuti kali lililomshinda kipa Sebwato Nichoklaus.

Huko mkoani Tanga, bao pekee lililofungwa na Salim Kipanga dakika ya kwanza ya mchezo liliiwezesha Mgambo Shooting kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya ndugu zao African Sports kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo, timu ya Majimaji ikicheza kwenye uwanja wake wa nyumbani ililazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara, Tanzania Prisons ikatoka suluhu na Mwadui FC kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya huku Kagera Sugar wakitoka suluhu na JKT Ruvu Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.

 

Imeandikwa na Mshamu Ngojwike, Jennifer Ullembo, Mwali Ibrahim na Oscar Assenga.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles