NA MARTIN MAZUGWA
MARA baada ya kupangwa kwa ratiba ya michuano ya Klabu Bingwa barani Afrika, wapenzi na mashabiki wa Yanga walianza kufurahia kupangwa na timu ngeni katika mashindano hayo kutoka Comoro.
Yanga wanatarajia kurusha karata yao ya kwanza ugenini katika visiwa vya Comoro Februari 10, ambapo watakuwa wageni wa Ngaya Club de Mbe, ambayo inashiriki mashindano ya kimataifa kwa mara ya kwanza tangu ilipoanzishwa mwaka 1992.
Klabu hiyo ambayo imekuwa moto wa kuotea mbali msimu huu wa Ligi Kuu ya Comoro (Comoro Premier League) na kuzitetemesha timu kongwe katika visiwa hivyo.
Furaha hiyo ya mashabiki inatokana na historia ya klabu hiyo pindi inapokutana na timu kutoka nchini Comoro, ambazo ndio kwanza zimeanza kuchipua katika mchezo wa soka barani Afrika na ulimwenguni kwa ujumla.
Wanajangwani wamekuwa wakibebwa na rekodi ya kikosi chao pindi wanapokutana na timu kutoka visiwa vya Comoro, ambazo zimeshindwa kufurukuta kwa miamba hiyo yenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani.
Je, safari hii Yanga wataweza kuendeleza ubabe wao mbele ya Wacomoro ambao hawajawahi kupata ushindi mbele ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania bara? Ni jambo la kusubiri na kuona mwisho wa vita hii iliyojaa kila aina ya msisimko.
Klabu ya Yanga inapaswa kuwa makini na kuacha kucheza mpira wa mazoea, hasa ukizingatia wanakutana na kikosi kilichobeba mataji matatu katika ligi ya Comoro, hivyo hawatakiwi kuwabeza.
Miaka ya karibuni mchezo wa soka umepiga hatua sana, rekodi zimekuwa zikivunjwa kila kukicha, hivyo wakali hao wa Jangwani wanapaswa kuwa makini juu ya hilo.
Yanga ambayo imewahi kupata matokeo ya kushangaza pale ilipowaangushia kichapo kikali Komorozine kwa kuifunga mabao 7-0, jambo linalofanya mashabiki wa klabu hiyo kuanza kupata kiburi cha kushangilia wakiamini kikosi chao kimepata mteremko katika hatua ya awali ya michuano ya klabu bingwa.
Wakali wa Jangwani wanapaswa kujiandaa vizuri, huku wakitumia uzoefu wa mkurugenzi wao wa ufundi, Hans van der Pluijm, pamoja na kocha mkuu, George Lwandamina, mwenye rekodi nzuri barani Afrika.
Lwandamina amejijengea jina lake msimu uliopita mara baada ya kuifikisha nusu fainali ya michuano hiyo ya Afrika timu ya Zesco na kuzifunga timu ngumu za Afrika Kaskazini ikiwemo miamba ya Misri, Zamaleck.
Licha ya kuwa na uzoefu, Lwandamina anapaswa kukiandaa kikosi chake vyema kwa michuano hiyo mikubwa barani Afrika, ili azidi kujenga heshima yake ambayo aliipata alipokuwa na miamba ya soka nchini Zambia, Zesco.
Yanga wanahitaji kufanya vizuri ili waweze kusonga mbele na kuepukana na jinamizi linalowakabili la kuishia hatua za awali, mara kwa mara katika michuano ya kimataifa.
Mabingwa hao watetezi wa ligi ya Tanzania, wanapaswa kujiandaa vizuri ili kuipeperusha vyema bendera ya taifa nchini Comoro na wakumbuke kuwa rekodi ziliwekwa ili zivunjwe.