24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

HOMA YA JANUARI INAVYOITESA MADRID

ADAM MKWEPU NA MITANDAO


INAWEZEKANA klabu ya Real Madrid ilikuwa na wakati mzuri wa mafanikio mwishoni mwa mwaka 2016, lakini tangu Januari mwaka huu imekuwa katika wakati mgumu ambao umewafanya kufanya vibaya katika baadhi ya michezo yao.

Timu hiyo imejikuta ikipoteza baadhi ya michezo yake muhimu baada ya kukumbwa na rundo la majeruhi katika kikosi chao.

Kocha wa timu hiyo, Zinedine Zidane, wiki iliyopita alishuhudia kikosi chake kikipata sare ya mabao 2-2 dhidi ya Celta Vigo  ambayo iliwaondoa katika michuano ya Kombe la Mfalme (Copa De Ray) na huo ukawa mwisho wa ndoto ya kunyakuwa mataji matatu msimu huu.

Mwezi huu umekuwa wa masikitiko makubwa kwa klabu hiyo baada ya kugeuza kila kitu chini juu na kufanya kampeni za klabu hiyo ya kunyakuwa ubingwa wa Ligi Kuu Hispania kuwa shakani.

Kwa sasa klabu hiyo inajipanga kubadili mwelekeo wa mwezi Januari ambao umekuwa mbaya hadi kuruhusu kuonekana dhaifu hata katika uwanja wa nyumbani wa Santiago Bernabeu.

Katika uwanja huo mwezi huu Madrid wamepoteza dhidi ya Sevilla katika michuano ya Kombe la Mfalme na  Granada katika mchezo wa Ligi Kuu ‘La Liga’.

Madrid wamefungwa na kutoa sare katika michezo yao miwili walipoitembelea Sevilla katika uwanja wa Estadio Ramon Sanchez Pizjuan na kupoteza asilimia 73 waliyokuwa nayo mwishoni mwa mwaka jana na kubakiwa na asilimia 42 ya kufanya vizuri mwaka huu.

Madrid imepotea baada ya kuvunja rekodi iliyowekwa na Barcelona kwa kucheza michezo 40 katika michuano yote bila kufungwa ikiwa juu ya wapinzani wao hao kwa mchezo mmoja.

Mbinu ya Zinedine zimeonekana kushindwa kufanya kazi tangu kuanza kwa Januari na kukaribisha kuandamwa na presha ya mashabiki wa Madrid.

Awali, Zinedine alikwa akifanya mabadiliko ya wachezaji yaliyofanya wapinzani wapate joto kali lakini kwa sasa kutokana na kuandamwa na majeruhi wengi hali imekuwa tofauti.

Eneo la ulinzi la Madrid limeonekana kuwa dhaifu na kuruhusu mashambulizi ya mara kwa mara yaliyochangia kufungwa jumla ya mabao matano katika michezo miwili dhidi ya Sevilla na mabao manne dhidi ya Celta Vigo.

Zaidi ni kwamba, Madrid imeathirika zaidi na adhabu ya kutosajili waliyopewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) hivi karibuni na huenda hiyo ikawa sababu ya wao kushindwa kuingia sokoni haraka ili kuinusuru timu hiyo ambayo kwa sasa imekuwa katika hali tete.

Kwa sasa kiwango cha James Rodriguez, bado kinaendelea kusuasua wakati Alvaro Morata akipoteza hali ya kujiamini hivyo kusababisha baadhi ya wachezaji kukosa sapoti kutoka kwao.

Tatizo la majeruhi mwezi Januari linawakumbusha wakati timu hiyo ikiwa chini ya Carlo Ancelotti ikielekea katika mchezo wa Kombe la Mfalme.

Madrid imekosa huduma ya Gareth Bale kwa muda wa miezi miwili na majeruhi ya Marcelo na Dani Carvajal, yanamfanya Zidane kuwa bila mbadala wa safu ya beki katika kikosi chake.

Kushuka kiwango kwa Cristiano Ronaldo, kumeonekana kuwa moja ya sababu ya kupotea kwa Madrid katika mwezi huu.

Nyota huyo wa Kireno alikuwa na msimu mzuri mwaka 2016 ambao alipata mafanikio makubwa katika maisha yake ya soka, lakini kwa sasa ameshindwa kuisaidia timu yake katika matatizo yanayoikumba ya kufanya vibaya katika michezo iliyocheza mwezi huu.

Lakini kadiri siku zinavyosonga nyota huyo anajaribu kurejea katika makali yake ingawa bado yupo katika wakati mgumu.

Licha ya kutolewa katika michuano ya Copa del Rey, Madrid inatarajia kuwa katika wakati mgumu mwezi ujao katika michezo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA) kutokana kuwakosa wachezaji muhimu katika kikosi chao.

Timu hiyo itakuwa na michezo miwili dhidi ya Napoli ambayo wasipokuwa makini pia wanaweza kutolewa.

Na endapo hali itaendelea kuwa mbaya wanaweza kuondoka katika mbio za  ubingwa wa La Liga msimu huu.

 Lakini bado Zidane ana muda wa kufanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake ili aweze kuikabili hali iliyojitokeza Januari hii.

Baada ya kushindwa kuinasa saini ya kipa wa Manchester United, Zidane ameonekana kutaka kuimarisha kikosi chake kwa kutumia ubora wa Pierre Emerick-Aubameyang.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles