25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA HAWATAACHA UNAFIKI

MAZUNGUMZO ya wapenda soka wengi wa Tanzania huwa yamejaa lawama, unafiki pamoja na kejeli na  hayo yanatokana na wengi wao waliopo kwenye familia hiyo kutopenda kujifunza kabla ya kuanza kuyazungumzia au kuyaelezea, huku wakiamini kukosoa peke yake ndiyo njia sahihi ya kuleta mafanikio.

Soka ni mchezo wa makosa na uwanjani kuna matokeo matatu kwa maana ya kufungwa, kushinda na kutoka sare, lakini pia kwa mchezaji mmoja mmoja kuna kufanya vizuri au kuchemka, hiyo inasababishwa na jinsi mchezaji anavyoamka, kikosi kilichopangwa na timu anayokutana nayo.

Yanga ni moja ya klabu kongwe nchini, ambayo inadaiwa kuongoza kwa kuwa na mashabiki wengi ndani na nje ya Tanzania, huku ikiwa imefanikiwa kutwaa mataji 26 ya Ligi Kuu Tanzania Bara zaidi ya nane kwa watani zao Simba.

Licha ya ukongwe wao kwenye soka, lakini timu hiyo inaongoza kwa kuwa na mashabiki na wanachama wanafiki, wanaochangia kuirudisha nyuma kimaendeleo.

Ukiachilia mbali wale viongozi wanaofanya unafiki kujipatia fedha kwa ‘big boss’, lakini kuna wale mashabiki ambao kazi yao kubwa ni kukosoa, huku wakiwa hawana mchango wowote ndani ya timu zaidi ya kupiga domo.

Mwanzoni mwa msimu huu, Yanga ilimsajili straika wa kimataifa kutoka Zambia, Obrey Chirwa, kwa lengo la kutaka kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji.

Mara baada ya michezo mitatu tu, mashabiki wa soka na viongozi wa timu walidiriki kusimama mbele ya vyombo vya habari na kueleza kuwa Chirwa ameletwa kwa ajili ya watu fulani kupiga fedha kutokana na kiwango kibovu alichokuwa akikionyesha.

Wapo pia waliodai mshambuliaji huyo aliyesajiliwa kwa zaidi ya Sh milioni 200 akiwa pia analipwa mshahara mkubwa kuliko wengine, ameonekana ‘kupwaya’  huku Katibu wa Baraza la Wazee la timu hiyo, Ibrahim Akilimali, akipigilia misumari kwa kusema: “Chirwa anaruka ruka tu uwanjani, fedha alizonunuliwa ni heri wangepewa wazawa”.

Ukimtoa Chirwa, lipo pia suala la kocha, George Lwandamina, aliyetokea Zesco United na kuvaa viatu vya Hans van Pluijm, ujio wake ulizua utata mkubwa kwa Wanayanga na kutengeneza sumu iliyoenea hadi sasa, kwani wapo watu wanaokosoa kila linalojitokeza kosa dogo na kusahau mazuri makubwa anayoyafanya.

Kwa sasa Lwandamina akipanga kikosi kikapoteza mchezo, Wanayanga wengi wanapaza sauti zao kwa kudai Mzambia huyo hana jipya ni heri akarejeshwa Pluijm, lakini inapotokea timu hiyo ikashinda sifa nyingi nzuri hupewa.

Ukimwangalia Chirwa waliyekuwa wanamtusi na kumpa majina ya ajabu na  hata maneno asiyostahili kupewa, hivi sasa anaonekana ndiye nguzo muhimu katika suala zima la kufunga.

Kwa sasa huwezi kusimama mbele ya Wanayanga na kusema Chirwa aondoke wakakuacha salama, hiyo inatokana na Mzambia huyo kupiga mpira mkubwa uwanjani, huku akiweza kuipa ushindi wa mara kwa mara timu yake kwenye mashindano mbalimbali kiasi cha wanachama kudiriki kusema ni heri wafungashiwe virago Amissi Tambwe na Donald Ngoma.

Kwa upande wa Lwandamina mara baada ya kupoteza mechi yao dhidi ya Simba, ikashindwa pia kupata pointi tatu kwa Mtibwa Sugar, Wanayanga walizungumza mengi ambayo kiuhalisia hawakustahili kusema, lakini jambo la  ajabu  na kuonyesha ni wanafiki na wababaishaji, Jumanne iliyopita kikosi hicho kikiwa na Lwandamina kiliweza kupata ushindi wa mabao 6-1 kwenye Kombe la FA,  mbele ya timu ndogo inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ‘Kiluvya United’, kila mmoja alionekana kumpongeza kwa kupanga wachezaji walioonyesha ushindani.

Ufike wakati Wanayanga wajifunze kupitia kauli za unafiki wanazotoa, hasa baada ya Chirwa na Vicent Boosou ambao walionekana si lolote si chochote kuwasuta, lakini kwa akili zao sitashangaa hata Yesu akirudi hawataweza kuacha unafiki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles