22.7 C
Dar es Salaam
Saturday, July 13, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga bingwa

Yanga bingwa*Ni baada ya Mwadui kuichapaSimba 

*Azam yaimaliza Kagera, Prisons yaiua Majimaji

NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

TIMU ya soka ya Yanga imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2015/16 na kutetea taji hilo baada ya mahasimu wao, Simba kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Mwadui FC jana katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Matokeo ya kipigo cha jana kwa Simba yalirahisisha kazi kwa Yanga ambayo ilikuwa ikisubiri ushindi katika mchezo ujao dhidi ya Mbeya City ili iweze kutangazwa mabingwa msimu huu.

Kwa mafanikio ya ubingwa msimu huu, Yanga sasa imefanikiwa kutwaa taji hilo kwa mara ya 21 na kuzidi kuwaacha watani wao wa jadi Simba ambao wamelinyakua mara 18 huku wakishindwa kufanya hivyo tangu msimu wa 2012/13.

Yanga wametangazwa mabingwa wapya msimu huu baada ya kufikisha pointi 68 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kwenye ligi huku ikiwa imebakiza michezo mitatu kukamilisha ratiba.

Kwa matokeo ya jana Simba imeshuka hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa imejikusanyia pointi 58, huku Azam FC ikipanda nafasi ya pili baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga na kufikisha pointi 60.

Simba sasa imebakiza mechi tatu kumaliza ligi ambapo kama itashinda zote itafikisha pointi 67 hivyo inaweza kumaliza ikiwa nafasi ya pili, lakini Azam imebakiwa na michezo miwili na inaweza kumaliza ikiwa na pointi 66 endapo itashinda zote.

Katika mchezo wa jana, timu zote zilianza kwa kushambuliana ambapo dakika ya 10, Haji Ugando wa Simba nusura afunge bao la kuongoza lakini shuti alilopiga na kumshinda kipa Jabir Azizi wa Mwadui liliokolewa na beki Iddy Mobby.

Mwadui walijibu shambulizi katika dakika ya 20 ya mchezo lakini shuti hafifu lililopigwa na mshambuliaji, Rashid Mandawa liliokolewa kwa urahisi na kipa wa Simba, Vincent Angban.

Dakika ya 23 kiungo wa Simba, Said Ndemla, alipiga shuti kali akiwa nje ya eneo la hatari lakini hesabu zake hazikukaa sawa baada ya mpira kupaa juu la lango la Mwadui.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo Mwadui walikosa bao la wazi baada ya Mandawa kushindwa kuunganisha vyema pasi ya Haji Sabato akiwa umbali wa sentimita chache kutoka langoni kwa Simba.

Bao pekee lililoipa ushindi Mwadui lilifungwa dakika ya 72 kupitia kwa Jamal Mnyate ambaye alitumia maarifa kuwatoka mabeki wa Simba na kuachia shuti lililotinga moja kwa moja wavuni.

Dakika ya 90 mwamuzi Anthony Kayombo kutoka Rukwa alimtoa nje kwa kadi nyekundu mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib, baada ya kumchezea rafu mbaya, Hassan Kabunda wa Mwadui.

Baada ya mpira kumalizika, mashabiki waliokuwa wamevalia jezi ya Yanga walimpa kocha wa Mwadui, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ mfano wa kombe lililofungwa bendera ya Yanga ambalo alilipokea.

Katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Kambarage, Kagera walianza kupata bao dakika ya 24 mfungaji akiwa ni Adam Kingwande ambapo Kipre Tchetche alisawazisha kwa upande wa Azam dakika ya 46 kabla ya Himid Mao kuandika bao la ushindi dakika ya 59.

Matokeo hayo si mazuri kwa Kagera kwani yamezidi kuiweka katika mazingira mabaya ya kushuka daraja msimu huu kutokana na kuendelea kushika nafasi ya tatu kutoka mkiani.

Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo uliochezwa katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya maafande wa Tanzania Prisons waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Majimaji FC ya Songea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles