24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga Bingwa 2014/2015

MASHABIKI YANGA (2)NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM
KLABU ya Yanga jana iliivua rasmi ubingwa timu ya Azam, baada ya kuichapa Polisi Morogoro mabao 4-1, katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kufikisha pointi 55, ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote, hivyo kuwa mabingwa wa michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2014/2015.
Ubingwa huo ni wa 25 kwa Yanga tangu kuanzishwa kwa michuano ya Ligi Kuu, huku ikiwaacha watani wao wa jadi, Simba waliochukua ubingwa huo mara 18, wakiwa wanahangaika kupata nafasi ya pili ili wajisitiri.
Mabao ya Yanga jana yalifungwa na Amiss Tambwe aliyepiga hat trick ya pili katika ligi na Simon Msuva.
Yanga walianza mashambulizi dakika ya kwanza kupitia kwa mshambuliaji Tambwe, aliyekosa bao baada ya shuti lake kutoka nje kidogo ya lango la Polisi, akiunganisha pasi ya Oscar Joshua na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Dakika ya nane Simon Msuva alikosa bao baada ya shuti lake alilopiga akiwa eneo la hatari kugonga mwamba na kurudi uwanjani na kuwahiwa na Kpah Sherman, lakini kichwa alichopiga kilipanguliwa na kipa na kuwa kona ambayo haikuwa na mafanikio kwa Yanga.
Seleman Kassim wa Polisi alijaribu kupiga shuti kali dakika ya 27, baada ya kuwatoka mabeki wa Yanga, lakini Dida aliudaka kiulaini kabla ya kukosa tena bao dakika ya 33 akipaisha juu mpira wa pasi safi ya Said Bahanuzi.
Bao la kuongoza la Yanga lilifungwa na Tambwe dakika ya 39, akipokea pasi safi ya Msuva na kupiga shuti la kiufundi akimtoka beki wa Polisi, Laban Kambole, hivyo kuwafanya Yanga watoke mapumziko wakiwa wanaongoza kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza huku Kocha wa Polisi, John Tamba, akimtoa Said Bahanuzi anayeichezea Polisi kwa mkopo akitokea Yanga dakika ya 51 na nafasi yake kuchukuliwa na Nicholaus Kabipe, mchezaji huyo alishangiliwa na mashabiki wa Yanga ambapo alikwenda kusalimiana na Kocha Hans van Der Pluijm na wachezaji waliopo benchi.
Dakika ya 52 Tambwe aliandika bao la pili kwa Yanga, akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Polisi kutokana na shuti kali la Msuva, kabla ya dakika ya 58 Ambrose kukosa bao la wazi akiwa amebaki na kipa, baada ya shuti lake alilopiga akiunganisha pasi ya Suleiman kupanguliwa na Dida.
Tambwe aliwanyanyua mashabiki wa Yanga kwa kufunga bao la tatu dakika ya 59, akimalizia kwa kichwa krosi safi iliyochongwa na Ngassa na kuondoka na mpira.
Msuva alifunga bao la nne kwa Yanga baada ya kuvunja mtego wa kuotea wa mabeki wa Polisi, akiunganisha pasi ya Ngassa, lakini wachezaji walimjia juu mwamuzi Zacharia Jacob kutoka Pwani kwa madai bao hilo si halali.
Dakika za 60 na 78 Polisi waliwatoa Meshack Abel na James Ambrose na kuwaingiza Nahoda Bakari na Mussa Mohamed, huku Yanga wakiwatoa Msuva na Tambwe dakika ya 75 na nafasi zao kuchukuliwa na Hussein Javu na Jerson Tegete na Niyonzima dakika 84 na kuingia Nizar Khalfan.
Polisi walipata bao la kufutia machozi dakika ya 83 kupitia kwa Bantu Admin, aliyepiga shuti la umbali wa mita 25 na kumshinda kipa wa Yanga na kugonga mwamba wa juu na kujaa wavuni.
Polisi ambao walichachamaa dakika za mwishoni, walikosa bao dakika ya 86, baada ya shuti la Kabipe alilopiga akiwa nje ya eneo la hatari, kupanguliwa na Dida na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Mashabiki wa Yanga walilipuka kwa furaha baada ya kipenga cha mwisho kulia, huku wakiwa wamebeba vikombe vya mfano wakizunguka uwanja wakiwa na wachezaji na benchi la ufundi wakiwa wamevalia jezi za ubingwa, wakiimba na kusherehekea.
Bao la Msuva latua Fifa
Wakati huo huo, bao alilofunga winga wa timu ya Yanga, Simon Msuva kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting, linatarajiwa kutumwa katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Yanga inalituma bao hilo Fifa ili kushindanishwa na mabao mengine duniani, kwa ajili ya kuwania Tuzo ya bao bora la mwaka huu ‘FIFA Puskas Award’, ambayo mwaka jana ilichukuliwa na staa wa Real Madrid, James Rodriguez.
Msuva alifunga bao hilo Ijumaa iliyopita, akichumpa hewani na kufunga kwa kichwa wakati timu yake ikishinda mabao 5-0, bao hilo limefananishwa na lile alilofunga Mholanzi Robin van Persie kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka jana, walipoichapa Hispania mabao 5-1.

Katibu Mkuu wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha, aliliambia MTANZANIA jana kuwa tayari wamekwishawasiliana na watu wa Azam TV wanaoonyesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom, ili kupata video ya bao hilo kabla ya kulituma Fifa.

“Japokuwa wenzetu wa Ruvu Shooting wanalilalamikia wakidai lilikuwa na mazingira ya offside (ameotea), sisi tumelichambua na tumeona mfungaji hakuwa ameotea. Naweza kusema kuwa lile ni bao la msimu na tutalituma Fifa,” alisema.

Tibohora alisema wanataka bao hilo liwe miongoni mwa mabao yatakayochambuliwa na Fifa kwa ajili ya kushindanishwa kwenye tuzo ya mwaka huu.

Hata hivyo, moja ya vigezo ambavyo Fifa huzingatia kwenye mabao hayo lazima bao liwe zuri (laweza kuwa shuti la mbali, tikitaka au jitihada binafsi za mchezaji), halitakiwi kuwa la kibahati, makosa au lililombabatiza mchezaji wa timu pinzani na kuingia wavuni.

Bao hilo pia lazima likidhi matakwa ya mchezo wa kiungwana ‘fair play’ (yaani mchezaji asiwe amekutwa na kosa lolote mchezoni na kukutwa na hatia ya kutumia dawa za kulevya), lakini Fifa hutoa tuzo hiyo bila kubagua ligi, jinsia au utaifa.
Yanga: Deogratius Munishi, Juma Abdul, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Kelvin Yondani, Said Juma, Simon Msuva/Hussein Javu, Haruna Niyonzima/Nizar Khalfan, Amissi Tambwe/Jerson Tegete, Mrisho Ngassa na Kpah Sherman.
Polisi: Abdul Ibad, Ally Teru, Hassan Mganga, Meshack Abel/Nahoda Bakari, Laban Kambole, Anafi Suleiman, Admin Bantu, Said Mkangu, Said Bahanuzi/Nicholaus Kabipe, Seleman Kassim na James Ambrose/Mussa Mohamed.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles