28.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Maofisa serikalini, wadau watakiwa kutoa ushirikiano

Dr-Florence-TurukaNa Adam Mkwepu, Dar es Salaam
JAMII, maofisa wa Serikali na wadau wengine wametakiwa kutoa ushirikiano unaotakiwa kwa kundi jipya la raia wa Marekani walioanza kujitolea hapa nchini.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Florens Turuka, ambapo alisema kuwa raia hao wa Marekani wanaojitolea wanahitaji kupewa moyo pamoja na msaada wa kiufundi watakaohitaji.
Alisema raia hao “wanatakiwa kusaidiwa kujifunza na kuzoea mila na kujifunza Kiswahili.”

Akizungumzia kuapishwa kwa raia hao wa kujitolea hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Dk. Turuka alisema wafanyakazi hao wana fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu watakapokuwa hapa nchini.
“Fanyeni kazi kwa bidii, fanyeni matendo mema, kuweni wavumilivu na shirikianeni vyema na Watanzania,” alisema.

Dk. Turuka, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, aliwashukuru wote walioshiriki katika matayarisho ya kundi hilo, ikiwa ni pamoja na familia walizofikia wakati wa mafunzo, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za kiserikali na wafanyakazi wa shirika la Peace Corps.

“Kitendo hiki kinathibitisha uhusiano mzuri na wa kindugu uliopo kati ya Tanzania na Marekani,” alisema.
Kazi za kujitolea za Shirika la Peace Corps ni za kihistoria, zikiwa zimeanza katika miaka ya sitini. Kundi la kwanza la kujitolea lilifika Tanzania mwaka 1962.

Kundi la watu 37 lililoapishwa hivi karibuni litafanya kazi katika sekta za afya na kilimo, likilenga maeneo ya elimu ya afya ya jamii na kilimo endelevu.
“Ni vyema tukakumbuka kuwa viongozi wetu waliweka misingi ambayo wananchi wa Tanzania na Marekani hatuna budi kuiendeleza,” alisema Dk. Turuka.

Alisema mpango huo unasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazokumba jamii katika masuala ya afya na kilimo.
“Mnasaida kuchangia na kusaidia juhudi za serikali kufikia malengo ya Milenia na Dira ya Maendeleo ya 2025 na MKUKUTA,” alisema.
Hafla hiyo ya kuapishwa ilihudhuriwa pia na Balozi wa Marekani hapa nchini, Mark Childress, Mkurugenzi wa Shirika la Peace Corps hapa nchini, Marion Elizabeth O’Malley na maofisa wengine wa serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles