25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga, Azam zategwa pabaya

YANGA-NA-AZAMNA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

DAU kubwa lililotajwa na mshambuliaji wa Tanzania Prisons, Jeremiah Juma anayewaniwa na klabu za Simba, Yanga na Azam FC, limewashtua viongozi na kuwafanya wazidi kusuasua katika uamuzi wa kunasa saini yake.

Nyota ya straika huyo iling’ara zaidi katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita baada ya kuifungia timu yake mabao 11 na kuisaidia kumaliza ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.

Kutokana na mafanikio yake msimu uliopita, Juma alifanikiwa kuingia katika kinyang’anyiro cha wafungaji bora na kushika nafasi ya sita baada ya mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe, kunyakua kiatu cha dhahabu kwa kufunga mabao 21.

Straika huyo aliyetoa changamoto kwa klabu za Simba, Yanga na Azam na kuanza kupigana vikumbo kuwania saini yake, aliliambia MTANZANIA jana kuwa tayari amemaliza mazungumzo ya awali na kutaja dau analotaka hivyo kazi imebaki kwa viongozi kufanya uamuzi wa mwisho.

“Mimi ni mwajiriwa wa Jeshi la Magereza, hivyo ili niweze kujiunga na klabu nyingine ni lazima nihakikishe masilahi yangu yapo vizuri na yanalindwa ipasavyo.

“Nimetaka kiasi ninachohitaji kwa klabu zote ambazo nimefanya nazo mazungumzo kwa lengo la kujiunga na timu zao, nitakuwa tayari kuichezea timu yoyote ambayo itaonyesha nia ya kunihitaji kwa kukubaliana na dau nililotaka,” alisema.

Hata hivyo, mshambuliaji huyo hakuwa tayari kuweka wazi dau analotaka huku akieleza kuwa anaamini ataweza kuchezea timu tofauti msimu ujao baada ya klabu moja kati ya hizo kudai ipo tayari kumlipa kiasi anachotaka.

“Ni wazi kwamba klabu zote tatu zinasuasua kwenye jambo hili, lakini nimepata matumaini kupitia kwa wakala wangu ambaye anasimamia kila kitu kuhusiana na suala hili,” alisema Juma.

Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga wanasaka saini ya straika huyo huku wakiwa tayari wamefanikiwa kumnasa kipa wa Prisons, Benno Kakolanya, aliyekuwa beki wa Simba, Hassan Ramadhani ‘Kessy’, beki Andrew Vincent ‘Dante’ wa Mtibwa Sugar, kiungo Juma Mahadhi wa Coastal Union na mshambuliaji, Obrey Chirwa kutoka FC Platinum ya Zimbabwe.

Simba pia tayari imesajili wachezaji watano ambao ni Muzamir Yassin, Mohamed Ibrahim (Mtibwa Sugar), Jamal Mnyate, Emmanuel Semwanza (Mwadui FC) na Hamad Juma (Coastal Union).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles