31.2 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga, Azam kusaka ufalme wa Ligi

1*Simba yatafuta pa kutokea kwa Stand baada ya kipigo

NA JUDITH PETER, DAR ES SALAAM

VIGOGO wa soka nchini, Yanga na Azam FC, leo watashuka dimbani katika viwanja tofauti kuendeleza dozi ya vipigo katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, huku majeruhi, Simba wakisaka pointi muhimu zitakazorejesha heshima baada ya kipigo kutoka kwa watani wao wa jadi.

Vinara wa ligi hiyo, Yanga, wanafukuzana na Azam kwenye msimamo wa ligi, wakiwa na pointi 12, baada ya kucheza mechi nne, lakini wakitofautiana kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, watakuwa ugenini kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa ligi hiyo, wakitarajiwa kuchuana vikali na wenyeji wao, Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, huku wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kufungwa mabao 2-0 msimu uliopita kwenye uwanja huo.

Akizungumzia pambano hilo, Kocha Mkuu wa Yanga Mholanzi, Hans Van Der Pluijm, amesema mchezo huo unahitaji wachezaji wake kutumia akili nyingi uwanjani kuhakikisha wanavuna pointi muhimu, ambazo zitawawezesha kubaki kileleni mwa ligi hiyo.

“Hatuna shaka kwa upande wa maandalizi yetu kuelekea mchezo huo, kwani tangu kuanza kwa Ligi Kuu kikosi kimekuwa bora na matokeo yamekuwa mazuri ya kuridhisha, hivyo hatuna sababu ya kupunguza kasi tuliyoanza nayo,” alisema.

Kwa upande wa Azam, wenye rekodi nzuri ya kuchomoza na ushindi kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Azam Complex, watakuwa wenyeji wa Coastal Union, ambao walianza vibaya ligi hiyo kwa kufungwa mechi mbili na kulazimishwa sare mara mbili.

Upinzani uliopo Ligi Kuu msimu huu umeanza kumpa wasiwasi kocha Mwingereza, Stewart Hall wa Azam, ambao umemfanya aanze kuwatupia lawama baadhi ya waamuzi wanaochezesha, akidai wanavuruga viwango vya wachezaji wake uwanjani.

Simba wanakabiliwa na kibarua kigumu mbele ya Stand United, ambao wamejiimarisha nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi sita katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wekundu hao wa Msimbazi waliojikusanyia pointi tisa, wameshuka hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi baada ya Jumamosi iliyopita kupokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa mahasimu wao, Yanga.

Kocha Mwingereza wa Simba, Dylan Kerr, ambaye hesabu zake za ushindi zilivurugika na kuambulia kipigo dhidi ya Yanga, atalazimika kufanya kazi ya ziada kwenye safu ya ulinzi ambayo ilimwangusha katika mechi hiyo ili kuondoa makosa yaliyojitokeza.

Msimu uliopita Simba walishindwa kufurukuta mbele ya Stand United, baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani na baadaye kuambulia kipigo cha bao 1-0 katika mchezo wa marudiano, uliochezwa kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa maafande wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora, ambao wanautumia msimu huu, kutokana na kutokamilika kwa ukarabati unaoendelea Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

JKT Ruvu, ambao hawajaonja ladha ya ushindi katika mechi nne walizocheza, kwa mara ya kwanza kikosi hicho kitashuka dimbani chini ya kocha msaidizi, Aziishi Kondo baada ya Felix Minziro kudaiwa kuachia ngazi.

‘Wanalizombe’ Majimaji watawakaribisha Ndanda FC kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea, wakati mkoani Tanga Uwanja wa Mkwakwani unatarajiwa kuwaka moto pale timu za African Sports na Mgambo Shooting zitakapochuana vikali.

Maafande wa Tanzania Prisons ambao wamezinduka msimu huu wakinolewa na kocha Salum Mayanga, watakuwa wenyeji wa Mwadui FC kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, wakisaka ushindi mwingine nyumbani baada ya kushinda mechi mbili walizocheza uwanjani hapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles