TIMU ya Yanga leo inatarajia kuvaana na Azam katika mchezo wa Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar, unaotarajiwa kuwa na upinzani mkali na wakuvutia utakaochezwa Uwanja wa Amaan.
Mchezo huo unavuta hisia za wadau wengi kutokana na timu hizo kupishana pointi chache katika msimamo wa ligi Kuu Tanzania Bara, Azam ikiwa na pointi 35 kileleni ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 33 katika nafasi ya pili.
Azam ambayo ipo kundi B pamoja na timu ya Mafunzo na Mtibwa Sugar, inakutana na Yanga iliyopo katika kundi hilo siku moja baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Mtibwa, huku Yanga ikiitandika Mafunzo bao 3-0 katika mchezo wa ufunguzi.
Kabla ya mchezo wa leo, timu hizo zilishakutana Oktoba 17 mwaka jana katika mchezo wa ligi ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Hata hivyo, tangu Agosti mwaka 2008 Azam ilipoanza kucheza Ligi Kuu hadi Oktoba 17 mwaka jana, timu hiyo imekutana na Yanga mara 19, imetoka sare mara sita na kufanikiwa kupata ushindi katika michezo saba na kufungwa mara nne.
Julai 29 mwaka jana katika mchezo wa robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Azam ilitoka sare na Yanga katika muda wa dakika 90 na baadaye kulazimika kupiga penalti na mchezo kumalizika kwa Azam FC kushinda kwa jumla ya penalti 5-3.
Mbali na michezo hiyo pia wababe hao walikutana katika mchezo wa Ngao ya Hisani uliochezwa Agosti 22 mwaka jana, mchezo ambao ulimalizika kwa matokeo kuwa sare na kulazimika kupiga mikwaju ya penalti na Yanga kuibuka na ushindi wa penalti 8-7.
Akizungumza juu ya mchezo huo kocha mkuu wa timu ya Yanga, Hans van der Pluijm, alisema kwamba utakuwa mchezo mgumu kuwahi kushuhudiwa na mashabiki wa soka nchini.
“Ni mchezo mwingine mgumu kushuhudiwa na mashabiki wa soka nchini kutokana na historia ya klabu hizo mbili, hiyo inatokana na ubora na uimara wa timu hizi,” alisema Pluijm.
Pluijm alisema kikosi chake kipo tayari kuwakabili wapinzani wao, akieleza kwamba wana matumaini baada ya dakika 90 ushindi utakuwa wao.
Naye kocha mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema anatarajia kukaa na wachezaji kujadili kwa kina mchezo wa juzi dhidi ya Mtibwa Sugar kujua makosa na kuyasahihisha kabla ya kuvaana na Yanga.
Hall alisema kila mchezaji alisikitishwa na kiwango walichokionyesha kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar na kuahidi kujisahihisha katika mchezo dhidi ya Yanga.
“Kila mchezaji amesikitishwa na kiwango, wanajua kuwa hawakucheza vizuri na walifanya makosa, lakini kila mmoja amejipanga kuonyesha mchezo mzuri kesho (leo) dhidi ya Yanga ili kupata ushindi,” alisema.